HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 14 September 2017

MAHAKAMA YALALAMIKIWA NA MTUHUMIWA SETH

Na KaramaKenyunko, Glogu ya jamii
MSHITAKIWA Herbinder Seth leo ameileza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, bado hajapelekwa Hospital ya Muhimbili kutibiwa kama amri ya mahakama ilivyoagiza.

 Mshtakiwa Seth ameyasema hayo leo baada ya wakili wake wa utetezi, Melchisedeck Lutema kuileza mahakama kuwa bado mteja wake huyo anayeshtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha inayomkabili yeye na mwenzake James Rugemalira bado hajapelekwa Hospital ya Muhimbili 


mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Lutema ameomba upande wa mashtaka ueleze kwanini mshtakiwa hapelekwi hospitali, kwani katika mashauri yaliyopita  mahakama imetoa amri mara kadhaa zote zikielekeza mshitakiwa huyo apelekwe Hospitali ya Muhimbili lakini haijatekelezwa.ameiomba mahakama itumie busara ili kuhakikisha mshtakiwa anapekwa hospitali na kwamba wakuthibitisha kama ametibiwa au la ni mshtakiwa mwenyewe.

Habinder amedai hayo baada ya Wakili wa Serikali, Leonard Swai akisaidiana na Vitalis Peter kudai kuwa shauri limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

akiongea kuhusu matibabu, alidai mshtakiwa alipelekwa hospital ya magereza na kwamba alitibiwa na mtaalamu Dotto Pakacha ambaye anampatia matibabu kila anapolalamika huwa wanamuona na kwamba yeye mwenyewe alifuatilia kupata uhakika kuwa anapatiwa matibabu kwani hata akipata shinikizo la damu huwa wanamuona.


"Tunaendelea na upelelezi kwasababu kuna mashtaka ya kugushi yanahusisha taasisi zaidi ya moja tunaomba mahakama itupe muda ili tukamilishe upelelezi"alidai


Hata hivyo, Hakimu Shaidi amesisitiza mshitakiwa Seth apelekwe katika hospitali ya Muhimbili kama ilivyotoa maagizo awali na kwamba inaonyesha wazi amri ya mahakama haifuatwi, “ oda ya mahakama lazima ifuatwe, haiwezekani kila siku tukija hapa tunaongea kitu kimoja tu hii haipendezi" amesema hakimu Shaidi.


Aidha, Wakili anayemtetea James Rugemarila, Pascal Kamala amedai kuwa washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo juni 19 mwaka huu hadi leo ni siku 87 wako ndani na makosa wanayoshtakiwa nayo hayana dhamana na upelelezi haujakamilika, ili haki iweze kutendeka kwa pande zote mbili wanaomba upelelezi ukamilike mapema na haki iweze kutendeka.


Kesi hiyo itatajwa Septemba 29 mwaka huu. 


Seth  na Rugemarila wanakabiliwa na mashtaka  12 ya  uhujumu uchumi  kwa kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kighushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha  na kuisababisha hasara ya USD 22, 198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad