HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 11 September 2017

DAWASA ILIVYOJIPANGA KUIMARISHA MTANDAO WA HUDUMA ZA MAJI KATIKA JIJI LA DAR ES SALAAM NA MKOA WA PWANI.

SERIKALI inatekeleza  Programu ya miaka mitano ya Maendeleo ya Sekta ya Maji nchini (2016/21) ambapo pamoja na mambo mengine imekusudia kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikoa ya  Mikoa kutoka asilimia 86 hadi 95.

Taarifa ya Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji inaonesha kuwa Idadi ya wateja waliounganishiwa huduma hiyo imeongezeka kutoka 405,095 mwezi Machi 2016, hadi wateja 432,772 mwezi Machi, 2017 ambapo asilimia 97 ya wateja hao wamefungiwa dira za maji ili kulipia huduma ya maji kulingana na matumizi. 

Pamoja na ongezeko hilo la uzalishaji wa maji bado mahitaji ya maji ni makubwa katika maeneo ya Miji Mikuu ya Mikoa ikiwemo Jiji la Dar es Salaam, hatua iliyoilazimu Serikali kuwekeza katika miundombinu ya maji na kuzijengea uwezo mamlaka za maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama katika Jiji hilo.

idadi ya maunganisho kwenye mtandao wa majisafi ya Jiji la Dar es Salaam imeongezeka kutoka wateja 155,000 mwezi Machi, 2016 hadi kufikia wateja 182,721 mwezi Machi, 2017, kutokana na kuongezeka kwa makusanyo ya maduhuli ya mauzo ya maji kutoka Tsh. Bilioni 7.1 Machi, 2016 hadi Tsh. Bilioni 8.3 Machi, 2017.

Akizungumza na Waandishi wa habari hivi karibuni Jijini Dar es Salaam, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi  Romanus Mwang’ingo anasema mamlaka hiyo inatekeleza miradi mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji maji, kusambaza maji maji katika Jiji La Dar es Salaam na baadhi ya Miji ya Mkoa wa Pwani.

Mwang’ingo anasema mahitaji ya maji katika eneo la huduma la DAWASA ikijumuisha miji ya Kibaha na Bagamoyo ni mita za ujazo 544,000, ambapo uzalishaji wa rasilimali hiyo kutoka vyanzo vya visima na mitambo ya Ruvu Juu, Ruvu Chini na Mtoni ni mita za ujazo 502,000 kwa siku.

Anaongeza hadi sasa Mamlaka hiyo tayari imekamilisha miradi mbalimbali inayokusudia kuongeza hali ya upatikanaji maji Jijini Dar es Salaam ikiwemo upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini uliowezesha kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maji kutoka lita za ujazo 180,000 hadi 270,000.

“Katika mtambo wa maji wa Ruvu Chini pia tumefanikisha ulazaji wa bomba kuu la mita 1.8 kutoka Ruvu chini hadi matenki ya chuo kikuu cha Ardhi, vilevilw kuanza ujenzi wa ofisi za kuendeshea mradi huu” anasema.

Kuhusu Mtambo wa Ruvu Juu, anasema DAWASA imekamilisha ujenzi wa njia mpya ya umeme mkubwa kutoka Chalinze hadi Mlandizi pamoja na kuongeza kiwango cha uzalishaji wa maji kutoka lita 82,000 hadi lita 196,000.

Kwa mujibu wa Mwang’ingo anasema ili kuhakikisha kuwa kiwango cha maji kilichoongezeka kinawafikia wananchi, DAWASA inatekeleza mradi wa uboreshaji wa mfumo wa usambazaji maji katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.

Akifafanua zaidi anasema kazi zilizofanyika katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa matenki 9 ya kuhifadhi na kusambaza maji yenye ukubwa wa kuhifadhi maji lita milioni 3 hadi 6, ujenzi wa vituo nne vya kusukuma maji pamoja na ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji yatakayokuwa na urefu wa kilometa 477.

“Maeneo yatakayonufaika na mradi huu ni pamoja na Salasala, Bunju, Wazo, Makongo, Changanyikeni, Bagamoyo, Mpiji, Zinga, Kiromo, Kitoprni, Ukuni, Kerege, Buma, Mataya na ukanda maalum wa EPZA” anasema.

Mhandisi Mwang’ingo anasema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuimarisha mitandao ya maji kuwa katika mfumo rasmi na hivyo kufanya maji kugawanywa kwa ufanisi na uwiano mzuri zaidi hususani katika maeneo ya milimani ambapo maji hayakuweza kuwafikia wananchi wengi.

Kwa mujibu wa Mwang’ingo anasema katika kudhibiti upotevu wa maji, DAWASA itafunga mita maalum katika maeneo ya kupokea maji na matoleo yake hatua inayolenga kujua kiasi kamili cha maji kilichoingia katika eneo husika na kiasi kilichogawanywa kwa wananchi.

“Tofauti na mita za kawaida, mita hizi zitakuwa zinapeleka taarifa moja kwa moja katika ofisi za DAWASCO ambapo vifaa maalum vitafungwa na itakuwa rahisi kutambua ni wapi maji yanapotea na hivyo kutafuta njia ya kuyadhibiti”

Kuhusu Miradi ya ukusanyaji na uondoaji wa majitaka anasema DAWASA imeanza mradi wa ujenzi wa mitambo mitatu mikubwa ya kusafisha majitaka itayojengwa katika maeneo ya Jangwani, Mbezi Beach na Kurasini hatua inayolenga kuongeza kiwango cha kusafisha majitaka kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2020.

Mhandisi Mwang’ingo anasema Gharama za jumla za miradi hiyo ni Dola za Marekani Milioni 600, ambapo miradi hiyo itatekelezwa kwa awamu na awamu ya kwanza inatarajia kuanza ndani ya mwaka huu wa fedha 2017/18.

Anasema mitambo hiyo mipya itawezesha kuzalisha gesi asilia na umeme utakaotumia kuendeshea mitambo, hatua itayosaidia kupunguza gharama za umeme na pia maji yatakayokuwa yametibiwa yatauzwa na kutumika katika shughuli mbalimali ikiwemo kupozea mitambo na umwagiliaji.

Akizungumzia kuhusu mradi wa uchimbaji visima katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Mwang’ingo anasema DAWASA imebuni mradi huo ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji katika baadhi ya maeneo ya Halmashauri Mpya ya Ubungo katika kipindi ambacho Manispaa hiyo ikisubiri utekelezaji wa miradi mikubwa ya usambazaji maji.

“Mradi utahusu uchimbaji wa visima 10 katika maeneo ya Kwa Mvungi, Gogoni, Mpiji Kibesa, Makabe-Mbezi Luis, Tegeta A, Matosa, Kingazi B, Malamba 2, Kingazi A, na Luguruni, ambapo uchimbaji visima umekamilika na mkandarasi anasafisha na kupima wingi na ubora wa maji” anasema.

Akiwasilisha Hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge anasema hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa na miji midogo imeendelea kuimarika na kuweza kupunguza kero ya uhaba wa maji safi kwa wananchi wa miji hiyo.

Waziri Lwenge anasema Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa miradi ya uzalishaji wa maji na miundombinu ya kusambaza maji ili kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo.

Anasema katika jitihada za kuimarisha vyanzo vya maji, Wizara yake imeendelea kuhamasisha wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji pamoja na utafutaji wa vyanzo vingine vya maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya kimkakati na uchimbaji wa visima virefu.

Serikali inatekeleza miradi mikubwa ya maji ili kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo ya kitaifa na kimataifa katika upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Ni wajibu wa wananchi kulinda miundombinu ya maji ikiwemo kudhibiti upotevu wa maji katika mifumo ya usambazaji wa maji kunakosababishwa na kuvuja kwa mabomba ya maji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad