HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 17 August 2017

TAKUKURU yampandisha mtendaji wa kijiji mahakamani kwa makosa matano

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nsimbo Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Deogratias Hanga amefikishwa Mahakama ya Hakimu wa Wilaya ya Tabora na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), akikabiliwa na mashtaka matano tofauti.
Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Edson Mapalala wa Takukuru ulidai mbele ya Hakimu Joctan Rushwela juzi kuwa mshtakiwa alighushi muhtasari wenye maelezo ya uongo kwa lengo la kujipatia Sh2.8 milioni kati ya Mei 12 mwaka 2015 na Januari 2016.
Ilidaiwa na Wakili Mapalala kuwa katika kesi hiyo ambayo ina washtakiwa wawili kuwa mshtakiwa akiwa ni mwajiriwa wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui aligushi muhtasari wenye maelezo ya uongo kwa lengo la kujipatia kiasi hicho cha fedha.
Katika shtaka la pili, tatu na la nne ilidaiwa na upande wa mashtaka kuwa Hanga aligushi mihtasari ya Juni,12 2017, Septemba 10, 2015 na Novemba 13, 2015 ikionyesha kwamba Paul John alihudhuria kwenye vikao vya Halmashauri ya Kijiji cha Nsimbo.
Shtaka jingine linalomkabili ofisa mtendaji huyo ni ufujaji na ubadhirifu wa fedha za mwajiri wake Sh2.8milioni alizokuwa amekabidhiwa.
Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Joha Shaban ambaye inadaiwa kuwa Mei 12, 2015 alimsaidia ofisa mtendaji huyo kutenda makosa hayo huku akijua kufanya hivyo ni kosa.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yao na walipelekwa rumande baada ya kukosa wadhamini hadi Agosti 22 mwaka huu shauri lao litakapoanza usikilizwaji wa awali kwani upelelezi wake umekamilika.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad