HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, August 7, 2017

NBS YAWATAKA WADAU WA TAKWIMU KUFUATA SHERIA NA TARATIBU ZA UTOAJI TAKWIMU.

Na Bushiri Matenda Na Agness Moshi - MAELEZO
Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS)  imetoa rai kwa wadau wa Takwimu Nchini kufuata kanuni na taratibu za utoaji takwimu ili kuepusha  sintofahamu baina yao, wapokeaji taarifa  na Taasisi husika .

Rai hiyo imetolewa na  Mkurugenzi Mkuu wa NBS Dkt. Albina  Chuwa  wakati akiongea na  Waandishi wa Habari  Jijini Dar es Salaam leo kufuatia taarifa zisizo sahihi zilizotolewa na  Kampuni ya Utafiti ya Geopoll yenye  ofisi ya Kanda ya Afrika, mjini Nairobi, Kenya kuhusiana Viwango na Idadi ya watazamaji wa vituo mbali mbali  vya habari vinavyorushwa hapa nchini .

“Taarifa zozote zinazohusu utafiti ni  lazima zihusishe wadau mbalimbali, na kwa kuzingatia vigezo vyote vinavyotakiwa na mamlaka iliyoidhinishwa kisheria kuhusiana na utoaji takwimu”, Dkt.Chuwa alivitaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na uwazi na ukweli, uhusishwaji wa Wadau na kwa kuzingatia weledi.

Aidha, amefafanua kuwa ni vyema Taasisi yoyote inayotaka kukusanya taarifa mbalimbali za takwimu ni budi kushirikisha wahusika ili kuepusha mkanganyiko na upotoshwaji kama ilivyofanywa na Kampuni hiyo kutoka Nairobi, Kenya.

“Takwimu zinazotolewa bila kuzingatia taratibu zinazohitajika hazitatambulika na Serikali kwani utoaji wa Takwimu haufanywi kama unavyohesabu migomba shambani, hivyo ni lazima wahusika wafuate  taratibu zote”, alifafanua Dkt.Chuwa.

Dkt.Chuwa amesema, Serikali haitambui Takwimu zilizotolewa hivi karibuni kupitia mitandao ya kijamii kwani hazikufuata Sheria ya Takwimu na hazijakidhi vigezo rasmi vya Takwimu na hivyo kuathiri mahusiano ya kiutendaji baina ya vyombo vya habari hapa nchini.

Kufuatia tukio hili, Ofisi ya Takwimu nchini inapenda kuzijulisha Taasisi zinazojihusisha na utoaji wa taarifa zinazotokana na utafiti nchini kwamba kwa mujibu wa Sheria ya 2015 NBS imepewa mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu upatikanaji wa takwimu kwa ajili ya matumizi ya Serikali na Wadau wa Takwimu.

Amesema, kwa mujibu wa Kifungu cha 6 cha Sheria hiyo, kinaipa NBS jukumu la kutoa na kusimamia miongozo na viwango vya utoaji rasmi wa Takwimu. “Hapo awali Ofisi ya Taifa ya Takwimu haikua na meno lakini mara baada ya marekebisho ya Sheria hiyo, sasa inayo meno ya kuiwezesha kudhibiti utoaji holea wa Takwimu nchini” Amesisitiza Dkt. Chuwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa amewataka Waandishi wa Habari kuacha kuandika taarifa ambazo hazijathibitishwa na NBS, pia ambazo hazina mashiko kwa Wananchi na Serikali kwa ujumla.

“Vyombo vya habari nchini viache kushabikia taarifa zinazotolewa na Taasisi zozote zisizo tambulika na kuthibitishwa na NBS hususani katika maswala ya Takwimu”, alisisitiza Bi. Zamaradi.

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015.  Kwa mujibu wa Sheria hiyo, NBS imepewa mamlaka ya kutoa, kusimamia  na kuratibu upatikanaji wa Takwimu rasmi kwa ajili ya matumizi ya Serikali na Wadau wa Takwimu.
Mkurugenzi mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Habari maelezo Jijini Dar es Salaam , kushoto Bw. Ephraim Kwisigabo Mkurugenzi Sensa na Takwimu za jamii.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad