Na Mwandishi Wetu
IMEELEZWA
kuwa uwekezaji bora kwenye sekta ya elimu, ikiwamo miundombinu, maktaba
na walimu walio na sifa za kufundisha, itaongeza ufaulu na uelewa kwa
wanafunzi.
Hayo
yalisemwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa shule
ya St. Anne Marie, Jasson Rweikiza kwenye mahafali ya 18 ya wanafunzi
wa darasa la saba, yaliyofanyika shuleni hapo Mbezi kwa Msuguri.
Alisema
ili kuinua kiwango cha ubora wa elimu nchini, ipo haja ya kuzingatia
uwekezaji huo pamoja na kuboresha maslahi ya walimu kwa kuwa watapata
ari ya kufundisha.
"Shule
ikiwa na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia kama vile vifaa
vya kutosha, madawati, maji, maktaba, walimu wenye ari matokeo ni elimu
bora, wadau tuwekeze zaidi," alisema Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba
Vijijini na Mwenyekiti wa wabunge wa CCM.
Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Gradius Ndyetabula alisema shule binafsi ni muhimu
kwa kuwa zinatoa mchango wa elimu na kuongeza fursa kwa Watanzania.
Alisema
iwapo shule za serikali pekee zingeachiwa mzigo wa elimu vijana wengi
wangekosa fursa ya kujiunga na kuendelea na masomo, kutokana na uchache
wa shule za serikali.
Alieleza
shule hiyo imeshika nafasi ya 32 kitaifa matokeo ya darasa la saba
yaliyopita kati ya shule za msingi 16,350 na kwamba wanatarajia wahitimu
43 wa darasa la saba mwaka huu watafanya maajabu kwasababu maandalizi
waliyofanya ni mazuri.
Alisema
kwenye matokeo ya kidato cha sita yaliyotangazwa hivi karibuni, St Anne
Marie ilifanikiwa kuwa ya tano kwenye Mkoa wa Dar es Salaam kwenye
matokeo hayo lakini siri kubwa ni mfumo mzuri wa ufuatiliaji wa matokeo
ya wanafunzi kitaaluma kuanzia ngazi za chini.
Alisema
pia shule hiyo ilifanikiwa kuwa ya kwanza kwa Wilaya ya Ubungo jijini
hapa na hivyo kuziacha kwa mbali shule zaidi ya 11 zenye kidato cha tano
na sita wilayani humo.
Aidha,
alisema mbali na kushika nafasi ya tano kwa Mkoa wa Dar es Salaam,
shule hiyo ilifanikiwa kufaulisha wanafunzi 15 kwa daraja la kwanza,
wanafunzi 48 daraja la pili, wanafunzi 23 daraja la tatu na mwanafunzi
mmoja tu ndiye aliyepata daraja la nne.
“Dar
es Salaam kuna shule 56 zenye kidato cha tano na sita na nyingi
zinavifaa na zana za kufundishia hivyo sisi kupenya hadi kuwa namba tano
si jambo rahisi, sisi tumejipanga kwa walimu wazuri na mazingira bora
ya kusomea kama maktaba ya kisasa na tunaahidi kufanya maajabu kwenye
mitihani ijayo,” alisema Ndyetabula.
No comments:
Post a Comment