HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 30, 2017

MAKALA MICHEZO: BUSWITA NA OBI KOSA MOJA ADHABU TOFAUTI.



Na Honorius Mpangala 

Ilikuwa ni mwaka 2006 klabu ya Manchester United ilipofanya ujanja kumsainisha John Michael Nchekwube Obinna. Obi kama anavyojulikana na wengi akiwa klabu ya FK Lyn ya Norway alijikuta akiingia tamaa ya kuvaa jezi ya United na kuingia mkataba wa awali bila wakala wake na klabu yake kujua. 

Akili aliyoitumia Obi ni ya wachezaji wetu wa kiafrika ambao wana teswa na ile methali "tamaa mbele mauti nyuma".Akiwa mzaliwa wa mji wa Jos katikati ya Nigeria alianza safari yake ya soka katika klabu ya hapo nyumbani kwao ya Plateau United.

Akiwa Norway Obi alipotea ghafla katika klabu yake na kusemekana kuwa ametekwa. Kumbe iligundulika alikuwa na Watu wa Manchester United ndipo alifanya 'uswahili' wa kusaini kandarasi ya kuitumikia United. Baadae picha zikasambaa kwenye mitandao akiwa na jezi ya United.

Kwa mapungufu yaliyofanywa na United iliwafanya Chelsea,kupita njia halali ya kumsajili. Uhalali na uwazi walioutumia Chelsea ukaonekana kuwa Manchester walimlazimisha Obi na kutokana na ukubwa wa klabu yao alijikuta anashindwa kukataa kuichezea klabu yao.

Baada ya sakata kufikishwa mbele ya Uefa maamuzi yanatolewa kuwa Manchester United walimsajili Obi kwa njia zisizo sahihi. Hawakumtumia wakala wake walimteka kijana wa watu lakini katika mazingira ambayo hata klabu yake inasemekana walijua ila hawakutaka kuwa wawazi. Maamuzi yalimnufaisha Chelsea na hatimaye Obi mwenyewe kwa kinywa chake akasema nataka kucheza Chelsea na sio Manchester United. Akakazia kuwa huko nilisaini kwa kushinikizwa.

Hatimaye Obi akaanza kuitumikia Chelsea katika makubaliano ambayo ilitakiwa klabu ya Chelsea ilipe fidia kwa Manchester united. Fidia hiyo ni kutokana na mkataba wa awali ambao Mchezaji aliusaini kuitumikia United.

Katika sula hilo hilo la Obi lilifanana na kile walichokifanya Klabu ya Simba kwa mchezaji wa Yanga Pius Buswita. Akiwa ni kijana mwenye umri wa Miaka 21 tu subira ambayo ingempa heri anaiweka kando. Anaamua kutumia tamaa mbele ambayo inampa majibu ya mauti ya Soka lake. 

Alichokifanya Buswita sio kigeni kwa wanasoka wa Afrika.Ziko rejea nyingi ambazo unaweza kuzitumia katika kutatua au kulinganisha matukio kwa wachezaji wa kiafrika inapokuja suala la Usajili.

Wakati FIFA wakitoa Adhabu kwa Didier Kavumbagu ya kutocheza soka miezi sita baada ya kusaini Klabu mbili tofauti kule Vietnam. Sisi hapa Tanzania shirikisho lilimpa adhabu ya kosa la kuwa na mkataba na Prisons na kusaini Mbeya city Mchezaji Mohammed Mkopi.Adhabu ya Mkopi ilikuwa ni mwaka mmoja.

Wakati klabu ya Simba inampa 'kishika uchumba' Mbuyu Twite pale Kigali hawakufanya mazungumzo na klabu yake. Walichokifanya Simba ni kumwendea moja kwa moja Mbuyu.Wenzao Yanga wakaenda mbali zaidi Baada ya kugundua Mchezaji huyo alikuwa kwa mkopo katika klabu ya APR lakini ni Mali ya Fc Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika jiji la Lubumbashi.

Sakata la Mbuyu likamalizwa kwa Shirikisho kuwataka Yanga kuwalipa Simba Fidia ya Gharama walizoingia kwa Mbuyu na ndio uuwangana. Uungwana huo ndio waliotumia Uefa kumtambua Obi ni wa Chelsea na kuwataka walipe fidia ya gharama walizo tumia United kwa Obi.

Ikiwa ligi kuu Tanzania haijaanza Shirikisho lilitoa muda wa kupitia pingamizi mbalimbali. Pingamizi zilihusu wachezaji katika soko la usajili. Hatimaye TFF walipokea pingamizi nyingi zilizohusu klabu nyingi zile za madaraja ya chini na ligi kuu na pia hata vituo vya kulelea wachezaji.

Katika pingamizi zilizopelekwa TFF hakukuwa na pingamizi lililomhusu Pius Charles Buswita aliyesajiliwa na Yanga akitokea Mbao Fc .Baada ya siku kadhaa kupita na kufanyika kwa mapitio ya pingamizi kabla ligi haijaanza TFF wanatangaza kufungiwa kwa Buswita mwaka mmoja.

Wakiwa wanatekeleza moja ya vifungu vilivyowekwa na bodi ya ligi wako sahihi Kwa Adhabu ya mchezaji mwenye mikataba miwili timu tofauti. Lakini suala hilo linachukua sura tofauti na lile la Mohammed Mkopi aliyekuwa akiitumikia Prisons na mkataba ukiwa umebaki mwaka mmoja akaamua kusaini Mbeya city. Utofauti ninao usema hapa ni kwamba Buwita hakuwa mchezaji wa Simba kama ilivyokuwa Kwa Obi hakuwa mchezaji wa Manchester united ila alishikishwa kishika uchumba cha mkataba wa awali. Wakati simba wakifanya hayo Buswita alikuwa na mkataba na Mbao. Ukianza kufuata mnyoyoro wa makosa unagundua Simba walifanya mazungumzo na Buswita kimakosa. Yanga wao wakafanya kama Chelsea ikawa kama walivyofanya Kwa Mbuyu wakaenda Kufanya mazungumzo na Mbao wenye mkataba na mchezaji. 

Mbao wanamruhusu Buswita kusajiliwa Yanga halafu Simba wanaweka mezani mkataba wao wa kishika uchumba. Maamuzi yaliyofanyika Kwa Mbuyu ndiyo ingekuwa halali zaidi kwasababu waliotoa ruhusa ya kuuza ni klabu yake ya awali yaani Mbao na mkataba wa Mbao na Buswita ulikuwa TFF. Sasa anapoibuka mwingine kusema Nina mkataba nae unajiuliza uliingia nae mkataba lini na ulipata idhini ya klabu yake maana bado ana mkataba na klabu. Jibu linabaki kuelea kama ngalawa ya Mzee chipumu Nyasa.

Mbao wangeweza kusema tumemuuza Pius kwenda Yanga na kama ana meneja naye angesema nilishirikiana na klabu kumuuza Buswita kwenda Yanga. Hili linakuwa jibu tosha Kwa makubaliano ya Yanga na Mbao kuwekwa bayana. Halafu bodi inaanza kupitia makubaliano ambayo Simba wanasema waliingia na Buswita. Baada ya kubaini kuwa Mchezaji alishikishwa kishika uchumba pasipo klabu yake ya awali kutokujua na ilihali wana mkataba naye,hii ingeliweka jambo katila sura ya suluhu kati ya Simba na Mbao.

Iko wazi mchezaji anaruhusiwa kufanya mazungumzo na klabu yoyote kama amebakisha mkataba wa miezi Sita na klabu anayoitumikia.Kitendo cha Simba kufanya mazungumzo na Buswita kina rejesha mambo yaleyale waliyowahi kuyafanya Kwa Mbuyu ilihali mchezaji alikuwa na mkataba na Fc Lupopo. 


Kosa la Mkopi linaweza kutofautina na Buswita kwasababu Mkopi alikuwa na mkataba na Prisons. Wakati Buswita hakuwa na mkataba wowote unaomtambulisha kuwa ni mchezaji wa Simba pale Tff. Ifahamike kuwa mikataba yote ya wachezaji inakuwa sehemu mbili klabuni kwake na Tff. Sasa ukifika ofisi za shirikisho wao wanaweza kuwa rahisi kukupa mkataba wa Buswita na mbao na sio Mchezaji huyo na simba.


Mahakama ikiwa ni mhimili katika dola hupenda kutoa maamuzi Kwa kutumia rejea za Mashauri mbalimbali toka maeneo mbalimbali. Katika soka yapo mambo ambayo tunayaiga kutoka maeneo mbalimbali na yanatupa picha nzuri katika kuendesha soka letu. Utofauti wa kimaamuzi katika ligi moja na nyingine hutokea katika kanuni za ligi husika japo sheria za mpira zinabaki kuwa kama zilivyo.

Katika ligi hiyohiyo kanuni hizohizo ziliamua fidia kwa Mrisho Ngassa na Mbuyu Twite kama ilivyokuwa Kwa Obi na Chelsea yake.Fidia pia iliwahi kuwakuta Chelsea Kwa Birmingham city Kwa mchezaji Danny Sturridge ambaye Chelsea walilazimika kulipa baada ya kumchukua mchezaji huyo akiwa kinda toka Manchester city ilihali mmiliki halali alikuwa ni Birmingham city.

Fidia sio jambo geni hivyo Buswita angeweza kujitetea mbele ya kamati na kutoa maamuzi ya fidia. Lakini Kwa bahati mbaya kwake hakubahatika kuitwa mbele ya kamati na kuhojiwa.

Kanuni zetu ndio mwongozo wa maamuzi yetu Kwa kufuata misingi na taratibu za utoaji maamuzi baada ya kusikiliza pande mbili na kutazama makosa yaliko na kutoa adhabu stahiki.


0628449904

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad