HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 31, 2017

LEO KATIKA KUMBUKUMBU: NI YULE YULE WA MEI 18, SAID SUED 'SCUD'

PICHANI:  Mshambuliaji wa Yanga, Said Sued 'Scud', wanne kulia.


Tarehe kama ya leo, 1991, mshambuliaji wa Yanga, Said Sued 'Scud', alifunga bao pekee na la ushindi dhidi ya Simba kwenye mchezo wa raundi ya pili ya ligi daraja la kwanza(sawa na ligi kuu siku hizi).

Bao hilo la dk ya 59(14 kipindi cha pili) lilifuatia lile la mchezo wa raundi ya kwanza wa Mei 18 mwaka huo ambapo 'Scud' pia alifunga bao pekee na la ushindi dhidi ya Simba.

Mtangazaji wa mchezo huo, Ahmed Jongo wa Radio Tanzania Dar Es Salaam, alisikika akisema, "Gooooooo...ni yule yule wa Mei 18". Msemo huu ukajipatia umaarufu sana mitaani hasa pale mtu akirudia kufanya kitu alichowahi kukifanya hapo kabla.

Mabao haya yanamfanya Scud awe mchezaji pekee kufunga peke yake mabao pekee na ya ushindi katika mechi mbili mfululizo za watani wa jadi kwenye ligi ya Bara.

Dua Said wa Simba naye aliwahi kufunga kwenye mechi mbili mfulizo; 
Julai 17, 1993, Simba wakishinda  1-0, bao la dk ya 69 na 
Septemba 26, mwaka huo huo, Simba wakishinda 1-0 tena, bao la dk 13. Hata hivyo, mechi hizi zilikuwa za ligi tofauti; ya kwanza ilikuwa ligi daraja la kwanza na ya pili ilikuwa ligi ya Muungano.

Ligi ya Muungano ilikuwa muendelezo wa ligi ya Bara na ya Zanzibar na bingwa wake ndiyo alikuwa akihesabiwa kama bingwa wa Tanzania huku bingwa wa Bara na yule wa Zanzibar wakiishia kucheza Kombe la Kagame pekee. Hii ndiyo sababu FIFA wanaitambua Yanga kama bingwa mara 22 wa Tanzania badala ya mara 27 kama wanavyojitambua wao. Kwa sababu, mara tano kati ya 27 zao, walishinda ubingwa wa Bara ambao kuanzia 1982 mpaka 2003, ulikuwa hautaambuliki na FIFA.

JINA LA SCUD

Mwaka huo, 1991, kulikuwa na Vita ya Ghuba iliyosababishwa na Iraq chini ya Sadam Hussein kuivamia Kuwait. Majeshi ya umoja wa mataifa yakiongozwa na Marekani, yaliingilia kati kuing'oa Iraq, vita ikazuka.

Sadam Hussein alijivunia mabomu ya Scud ambayo yalikuwa tishio kweli kweli.

Katika mchezo wa 'kutesti mitambo' kati ya Yanga na Reli ya Morogoro uwanja wa Karume, Yanga walikuja na mtambo mmoja uliokuwa ukipiga mashuti kama mabomu ya Scud. Hapo ndipo mashabiki wakambatiza jina hilo mshambuliaji wao mpya ambaye alikuwa hafahamiki sana hapo kabla.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad