HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 14 August 2017

KAMATI YA OLIMPIKI TANZANIA YATOA MAFUNZO YA UTAWALA NA UONGOZI WA MICHEZO SIMIYU

  Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi(katikati) akizungumza na washiriki wa Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC) wakati alipofungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka Mjini Bariadi.
  Mkurugenzi Mkuu wa Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo kutoka Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC) Ndg.Suleiman Jabir akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo kutoka mkoani Simiyu (hawapo pichani) ambayo yanafanyikwa kwa muda wa siku tano Mjini Bariadi.
 Afisa Michezo wa Mkoa wa Simiyu,Ndg.Addo Komba (kushoto) akizungumza katika mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo kwa maafisa michezo, viongozi wa vyama vya michezo na walimu wa michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC).
 Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC) wakifuatilia Hotuba ya Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi(hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo hayo kwaniaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Mhe.Anthony Mtaka mjini Bariadi.
 Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi(wa tatu kulia walioketi) katika picha ya pamoja na maafisa michezo, viongozi wa vyama vya michezo na walimu wa michezo wa Mkoa wa Simiyu, wanaoshiriki wa Mafunzo ya Utawala na Uongozi wa Michezo mjini Bariadi ambayo yameandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC); (wa pili kulia) Mkurugenzi Mkuu wa Mafunzo Ndg.Suleiman Jabir
Mkurugenzi Mkuu wa Mafunzo ya Ndg.Suleiman Jabir Utawala na Uongozi wa Michezo kutoka Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC)(kulia) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Itilima, mhe.Benson Kilangi ambaye amefungua mafunzo hayo mjini Bariadi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, MheAnthony Mtaka.

Na Stella Kalinga, Simiyu
Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC) imeanza kutoa mafunzo ya siku tano ya Utawala na Uongozi wa Michezo Mkoani Simiyu, ambayo yamelenga kuleta tija katika kusimamia na kuendeleza Michezo.
Mafunzo hayo yanawahusisha Maafisa Michezo Mkoa na Wilaya, Viongozi wa Vyama mbalimbali vya Michezo  na walimu wa michezo kutoka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari mkoani Simiyu.
Mkurugenzi Mkuu wa Mafunzo hayo Ndg.Suleiman Jabir amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwasaidia Maafisa Michezo, viongozi wa vyama vya michezo ngazi ya mkoa na wilaya sambamba na walimu wa michezo kupata mafunzo ya kiufundi katika kusimamia na kuendeleza michezo, ambayo hutolewa katika mikoa yote hapa nchini, chini ya usimamizi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania(TOC).
Akizungumzia ushiriki wa wanawake Ndg. Jabir amesema Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) imehakikisha kuwa wanawake wanashiriki kwa asilimia 40 katika mafunzo hayo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa la mwaka 2016 la kuwashirikisha wanawake katika masuala muhimu ya kimichezo ikiwemo suala la uongozi.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Mhe.Benson Kilangi amesema, Utawala na uongozi wa michezo ulio bora ni msingi wa kuongoza na kuendeleza michezo  kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu.
“Kamati ya Olimpiki imeandaa mafunzo haya kwa wakati muafaka kwa sababu wanahitajika viongozi wenye taaluma ya kisasa ya namna ya kuongoza michezo na wanamichezo,ambao watakwenda na wakati kutenda kazi zao bila mgongano au vurugu “ amesema Kilangi.
Kilangi amewataka washiriki kuhakikisha kuwa wanazingatia mafunzo watakayopata na kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao, ili mafunzo hayo yasiishie tu katika Taasisi walizopo bali elimu hiyo ifike hadi ngazi ya vijiji ambako ndiko kwenye wachezaji wengi.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa washiriki kutumia mafunzo hayo kama chachu katika kufuata taratibu zote za uendeshaji wa vilabu na vyama vya michezo katika mkoa wa Simiyu ikiwa ni pamoja na kufuata katiba.
Ameongeza kuwa pamoja na kuchukulia michezo kama burudani na sehemu ya kuimarisha afya, washiriki hao wanapaswa kuwasaidia wachezaji kutumia michezo kama ajira inayoweza kuwaingizia kipato.
Kwa upande wake Afisa Michezo wa Mkoa, Ndg.Anthony Komba amesema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kusimamia michezo kwa weledi mkubwa, kuibua vipaji na pia yatasaidia vyama vya michezo kusimamia vema vyama vyao, ikiwa ni pamoja na kufuata katiba hali itakayowasaidia kuepuka migogoro katika vyama.
Mafunzo kwa Maafisa Michezo, viongozi wa vyama vya michezo Mkoa na Wilaya pamoja na walimu wa michezo kutoka katika baadhi ya shule za msingi na sekondari Mkoani Simiyu, yanafanyika katika ukumbi wa BARIDECO mjini Bariadi na yatahitimishwa siku ya Ijumaa tarehe 18/08/2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad