HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 28 August 2017

JKCI KUENDELEA KUPOKEA MADKTARI KUTOKA CHINA.

Na.Agness Moshi na Bushiri Matenda-MAELEZO.
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inatarajia kupokea madaktari wengine wanne kutoka China kwa ajili ya kuendelea kusaidiana na madaktari wazawa katika taasisi hiyo baada ya madaktari wengine wanne kutoka China kumaliza muda wao. 
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt.Peter Kisenge katika hafla ya kuwaaga madaktari wanne kutoka China waliomaliza muda wao wa utumishi hapa nchini ambao walikua wakishirikiana naTaasisi hiyo kwa takribani miaka miwili.  
“Wanarudi nchini China baada ya kumaliza muda wao, Tunawashukuru kwa kushirikiana nasi kwa kipindi chote walichokua nasi tunaishukuru Serikali ya China kwa misaada mbalimbali wanayotupatia ikiwemo ujenzi wa jengo la Taasisi ya Moyo, madaktari,wataalam pamoja na vifaa tiba”, alisema Dkt.Kisenge.
Dkt.Kisenge aliongeza kuwa hivi karibuni Taasisi inatarajia kupokea madaktari wengine wanne kutoka China kwa ajili ya kuendelea kushirikiana nao   katika utoaji huduma ili kuweza kuifanya Taasisi hiyo ya kimataifa.
Naye Kiongozi wa timu ya Madaktari kutoka China kwa Mkoa wa Dar Es Salaam Dkt.Sun Long amesema kwa miaka miwili waliyofanya kazi na Taasisi hiyo wamefanikiwa kufanya oparesheni  takribani 373 jambo ambalo limesaidia kupunguza  gharama za matibabu na idadi ya wagonjwa wa Moyo kwenda kutibiwa nje ya Nchi kama vile India.
“Sasa hakuna haja ya kutumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu ya Moyo, Matibabu yote yanapatikana katika taasisi hii, hakuna Matata, Hapakazi Tu”, alisisitiza Dkt. Long.
Aidha, Dkt.Long amesema kuna haja ya nchi hizi mbili kuendelea kushirikiana ili kuendelea kusaidiana katika utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kubadilishana wataalam ili kukuza uwezo katika utoaji huduma.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi wa jopo la madaktari waliomaliza muda wao Dkt. Gu Zhigiang ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kujitegemea katika matibabu ya magonjwa ya Moyo kwa wananchi wake na ameshukuru ushirikiano walioupata kutoka kwa taasisi hiyo kwa kipindi chote walichofanya kazi hapa nchini. 
“Ninamshuru kila mmoja na ninafurahi kuhudumia Nchi hii nzuri, ninatumaini tutaendelea kushirikiana zaidi”, alisema Dkt. Gu Zhigiang.
Dkt. Gu Zhigiang ameongeza kuwa anatarajia kukua kwa ushirikiano baina ya nchi hizi mbili kwani tunaelekea kuadhimisha miaka 50 ya ushirikiano kati ya Serikali ya China na Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad