HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, August 30, 2017

Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija.


Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.

Aidha Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha mkoa wetu unakua mahala salama. Hata hivyo kumekuwa na tukio moja la unyang’anyi wa kutumia silaha wilaya ya Chunya kama ifuatavyo :-

Mnamo tarehe 29.08.2017 majira ya saa 06:00hrs katika kitongoji cha Logia, kijiji na kata ya Upendo, tarafa ya Kiwanja wilaya ya Chunya, mkoa wa Mbeya, dereva HERI ELIA RUBIENO [32], mkazi wa Ilemi – Mbeya akiendesha gari T.767 DDN aina ya Isuzu basi la abiria liitwalo SAFINA mali ya ISAYA SAMWEL MTITU, mkazi wa Njombe ikitokea kijiji cha Mamba kwenda Mbeya mjini njiani ilizuiwa na watu wapatao sita ambao waliweka magogo njiani wakiwa na silaha bunduki moja idhaniwayo kuwa ni shortgun na silaha nyingine za jadi [panga, rungu, na shoka]

Katika tukio hilo abiria waliporwa simu aina mbalimbali zenye thamani ya Tshs 410,000/= pamoja na pesa taslimu Tshs 2,771,000/=. Aidha wakati wa tukio abiria kadhaa walipata michubuko na mikwaruzo na walipatiwa matibabu katika zahanati ya Makongolosi na kuruhusiwa. Watu hao mara baada ya tukio walifyatua hewani  risasi mbili na kutokomea kusikojulikana kwa kutumia usafiri wa pikipiki.

Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata majambazi watatu ambao pia walitambuliwa na wahanga pamoja na pikipiki moja MC 388 BFZ aina ya Kinglion. Watuhumiwa hao ni

i.    JUAKALI MBALAMWEZI [65], mkazi wa Sumbawanga
ii.    GASPAR MAHINI [22], mkazi wa Sumbawanga
iii.    PETRO JUMA [21], mkazi wa kijiji cha Mamba [A].

Ufuatiliaji zaidi kuhusiana na tukio hili bado unaendelea ikiwa ni pamoja na kuwakamata watuhumiwa wengine pamoja na silaha.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu  Kamishna wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA  anatoa  wito kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria, badala yake wahakikishe wanawafikisha katika mamlaka husika watu wanaowakamata kwa tuhuma mbalimbali ili sheria ichukue mkondo wake.

 Aidha Kamanda MPINGA  anatoa rai kwa yeyote mwenye taarifa juu ya  watu wengine waliohusika katika tukio hilo  azitoe katika mamlaka husika ili wakamatwe na sheria ichukue mkondo wake vinginevyo wajisalimishe mara moja. Pia anatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwa na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka kwa kutumia njia mkato zisizo halali, badala yake wafanye kazi halalli ili kupata kipato halali.

Pia  Kamanda MPINGA anawatakia Heri ya sikukuu ya EID EL HAJI wakazi wa Mkoa wa Mbeya washerehekee kwa amani na utulivu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi. Watumiaji wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara wazingatie  Sheria za usalama barabarani.

[MOHAMMED R. MPINGA - DCP]
 KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad