HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 23 August 2017

Hakuna mgogoro wowote pori Tengefu la Mkungunero-DC Kondoa

Na Mwandishi Wetu, Kondoa 

BAADA ya baadhi ya vyombo vya habari kutangaza kuwepo mgogoro kati ya wananchi na serikali katika Pori tengefu la Mkungunero wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma, mkuu wa wilaya hiyo amejitokeza na kudai taarifa hizo hazina ukweli.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bibi Sezaria Makota, alisema habari zilizosambazwa kuhusiana na wananchi kunyanyaswa katika pori la Mkungunero zinazungumzia matukio ya zamani ambayo kimsingi yameshapatiwa ufumbuzi na serikali.

“Katika taarifa zilizotolewa kwenye vyombvo vya habari imeelezwa kuwa viongozi na wanakijiji katika Kijiji cha Kisondoko na Kata ya KK kuwa wananyanyaswa na kuna wasichana walisema wamebakwa lakini nakanusha taarifa hizi si za kweli, wafanyakazi wa pori la Mkongonero wanajiheshimu na wanafanya kazi kwa nidhamu,” alisema Bi. Makota na kuongeza:

“Nilipofika Kondoa mwaka jana (2016) nilisikia hayo malalamiko lakini nilipofuatilia nikabaini si kweli, viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama waliitisha mkutano kuwahoji wanakijiji wanaosema walinyanyashwa, kupigwa na kubakwa, kulikuwepo na madaktari waliowafanyia vipimo lakini hakuna aliyeonekana amebakwa.”

Katika maelezo yake Bi. Makota aliweka wazi kuwa ni kweli wanahabari walifika ofisini kwake kumhoji kuhusiana na manyanyaso wanayofanyiwa wakazi wa Kijiji cha Kisondoko, wakafanya mahojiano pia na meneja wa poro hilo, lakini taarifa zao hazikutolewa kwenye vyombo vya habari bali zimetolewa za upande mmoja kinyume na maadili ya uandishi wa habari.

“Waandishi wa habari walimuhoji meneja wa pori la akiba la Mkongonero na wakanihoji mimi lakini mbona tuliyozungumza hawakuyatoa kwenye vyombo vya habari,” alihoji Bi. Makota na kuongeza: “Njilimuuliza (mwandishi ambaye hata hivyo hakumtaja jina) umekuta wananchi wangapi wameumizwa, wangapi wamenyanyaswa au kubakwa, akasema amehoji tu wananchi kwa ujumla. Nikamwambia arudi akawahoji walioumizwa na waliobakwa lakini hadi sasa hajarejea.”

Akizungumzia ziara ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani, Bi. Makota alisema Agosti 8, 2016 naibu waziri huyo alipotembelea wilaya yake wananchi waliibua suala hilo la manyanyaso lakini walipotakiwa kujitokeza waliofanyiwa vitendo hivyo hakuna aliyejitokeza kutoa ushuhuda.

Hata hivyo, mkuu huyo wa wilaya alikiri matatizo hayo kutokea lakini ilikua masuala ya zamani ambayo tayari yameshapatiwa ufumbuzi, hata viongozi wa kijiji hicho walikiri kuwa wananchi walikua wakikumbukia mambo yaliyotokea zamani si kwa wakati huu.

“Kijiji cha Kisondoko ni miongoni mwa vijiji vilivyoanzishwa ndani ya pori hili tengefu, lakini wananchi wanaishi vizuri na tayari wameshatambua mipaka yao. Lakini wapo wananchi wanaotaka kujaribu kuvuka mipaka na hao ndio wanaozusha habari hizi zisizo na ukweli, kwa nafasi yangu nitahakikisha sheria inafuatwa na kulinda mipaka kwa mujibu wa taratibu za uhifadhi,” alisisitiza Bi. Makota.

Tangu kuanzishwa kwa poro tengefu la Mkungunero wilayani humo kumekuwepo na mvutano kati ya askari wa pori hilo na wananhi kutokana na madai kuwa wananchi wanataka kuingilia mipata ya pori, hata hivyo viongozi kwa muda mrefu wamekuwa wakifuatilia kwa karibu mgogoro huo na unaonyesha kuwa na tija. Mwisho

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad