Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson (mwenye baiskeli wa pili kulia) akiwa na viongozi wa Mkoa na baadhi ya Wabunge wa Mkoa wa Simiyu na Viti Maalum kutoka nje ya Mkoa kwa ajili ya kufungua mashindano ya baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi.
Na Stella Kalinga, Simiyu
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amefungua
Mashindano ya Mbio za Baiskeli na Ngoma za Asili Mjini Bariadi(Simiyu Jambo Festival) ambayo
yamehudhuriwa na Maelfu ya Wananchi wa Mkoa wa Simiyu.
Mashindano hayo ya mbio za baiskeli yamehusisha kilometa 200 wanaume, kilomita 80 wanawake ambapo
pia walemavu waliweza kushindania katika umbali wa kilomita tano.
Akizungumza baada ya kufungua mashindano hayo Dkt.Tulia pamoja na kuupongeza Mkoa wa Simiyu
kuandaa mashindano hayo amesema, ipo michezo nchini haijapewa kipaumbele lakini ikitumiwa vizuri
inaweza kutoa ajira ukiwemo mchezo wa mbio za baiskeli; ambapo ametoa wito kwa viongozi wa mikoa
mingine pia kuwekeza katika michezo mbalimbali ili kuwasaidia wananchi kupata kipato.
Washiriki wa mashindano ya mbio za Baiskeli kilometa 200(wanaume) wakiendelea kuchuana vikali kushindania pikipiki na fedha taslimu.
“Lililofanyika Simiyu ni jambo jema sasa watu watakuwa wanajua kuwa wakijifua vizuri kwenye baiskeli
na ngoma za jadi wanakuja kushiriki mashindano ya Baiskeli Simiyu, nitoe wito kwa viongozi wengine
kufikiria mambo mengine yanayoweza kuwasaidia wananchi katika maeneo yao kupata ajira na kujipatia
kipato” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema mkakati wa mkoa huo ni kurasimisha tamaduni
zote za Mkoa wa Simiyu na kuhusianisha na shughuli za Utalii ndani ya mkoa huo.
“Position(Nafasi) ya Mkoa wa Simiyu kwenye nchi ni kukuza tamaduni na sanaa zetu kama moja ya eneo
litakalotuunganisha na sekta ya Utalii, tumezungukwa na mapori ya akiba na mbuga za wanyama,
tungehitaji watalii wanapokuja kwenye maeneo hayo wapate ladha ya tofauti kiwemo utamaduni wa
Mtanzania”.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson (wa pili kushoto) akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza kilometa 200 (wanaume), Hamisi Hussein kutoka Arusha katika mashindano ya Baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi (kulia) ni Mkurugenzi Kampuni ya Jambo Food Products ambayo ni mdhamini, Mhe.Salum Khamis akimpongeza Mshindi huyo
Mtaka ameongeza kuwa wasanii wote watatambuliwa na baadae kujengewa uwezo kupitia watalaam wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(Kitivo cha sanaa),Chuo cha Sanaa Bagamoyo na vyuo vya michezo ili
waweze kufanya kazi zao kibiashara na kuimarisha uchumi wao.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Jambo Food Products,Mhe.Salum Khamis ambaye ndio
Mdhamini wa mashindano ya Baiskeli na ngoma za Asili (Simiyu Jambo Festival) amesema ataendelea
kudhamini mashindano kama hayo Mkoani Simiyu ili kuwaweseha wananchi kuinua kipato kupitia vipaji vyao.
Naye mshindi wa kwanza mbio za kilometa 80 (wanawake) Raulensia Luzuba kutoka Mwanza ameomba
mashirika na makampuni mbalimbali kuwadhamini ili waweze kujengewa uwezo na kuandaliwa kushiriki
katika mashindano ya Kimataifa.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson akiwa katika picha ya pamoja na washindi watatu wa mbio za Kilometa 10 (walemavu) na viongozi wa Mkoa wa Simiyu na baadhi kutoka nje ya mkoa wa Simiyu, mara baada ya kumalizika kwa mashindano ya baiskeli na Ngoma za Asili(Simiyu Jambo Festival) Mjini Bariadi.
Masunga Duba mshindi wa mbio za kilometa 200(wanaume)kutoka Simiyu amesema pamoja na wafadhili
kudhamini mashindano ameomba pia wawasaidie wachezaji kupata baiskeli za kisasa zitakazowasaidia
kwenda kwa kasi inayotakiwa.
Mashindano ya baiskeli Mkoani Simiyu yameshirikisha wachezaji kutoka mikoa ya Simiyu, Mwanza,
Shinyanga,Arusha na Mbeya ambapo ushindi kwa upande wa wanaume umechukuliwa na Hamisi
Hussein(Arusha) ambaye amejishindia pikipiki, wa pili ni Masunga Duba(Simiyu) kitita cha shilingi
1,000,000/= wa tatu Richard Laizer .shilingi 500,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa
nne mpaka wa 15.
Kwa upande wa wanawake mshindi wa kwanza Raulensia Luzuba kutoka Mwanza amejipatia shilingi
500,000/=, mshindi wa pili Tatu Malulu(Mwanza) shilingi 400,000/= na wa tatu ni Vumilia
Mwinamila(Simiyu) shilingi 300,000/= na zawadi nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne mpaka wa 10.
Walemavu mshindi wa kwanza Emmanuel Mtemi amejipatia shilingi 200,000/= wa pili Masunga Sendama
shilingi 150,000/= na wa tatu Saguda Sospeter shilingi 100,000/=wote kutoka mkoa wa Simiyu na zawadi
nyingine zimetolewa kwa mshindi wa nne na wa tano.
Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson akimkabidhi ufunguo wa pikipiki mshindi wa kwanza (wanaume) katika mashindano ya Baiskeli yaliyofanyika Mjini Bariadi kilometa 200, Hamisi Hussein kutoka Arusha.
No comments:
Post a Comment