HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, August 31, 2017

⁠⁠⁠ASANTE KUWA NAHODHA LIPULI SIO 'STORY' ILA BOCCO KUWA NAHODHA SIMBA 'STORY'.






Na. Honorius Mpangala.

Ilikuwa ni katika mchezo wa ligi kuu kati ya Yanga dhidi Lipuli nilipomwona Asante kwasi akiwa amevaa 'usinga' wa nahodha. Pale pale kuna vitu vikaanza kunifikirisha nikijaribu kurejea kwenye kauli za wadau na wapenzi wa soka letu.


 Kauli ambazo zinifanya akili izame huko ni katika kumbukumbu ya maneno yaliyotolewa baada ya benchi la ufundi la Simba kunadili uongozi wa wachezaji. Maneno yalikuwa dhidi ya John Rafael Bocco kupewa unahodha msaidizi nyuma ya Method Mwanjale na Mohammed Hussein. Ilikuwa katika kambi ya klabu ya Simba nchini Afrika kusini ambapo benchi la ufundi liliamua kubadili uongozi wa wachezaji. 

Mabadiliko yalifanya Method Mwanjale kuwa nahodha badala ya Jonas Gerrard Mkude na kupewa wasaidizi wake .Katika orodha ya wasaidizi ilikuwa jina la John Rafael Bocco ndilo lililowafanya wapenzi na wadau walitolee hoja tofauti.

 Maswali yalikuwa kwanini Bocco na sio Kazimoto au wengine waliokuwepo klabuni hapo Kwa muda mrefu. Ilichukuliwa kama ni kitu cha kushangaza sana katika tukio lile. Sababu kubwa ilikuwa kutokana na Kuvuliwa unahodha huo mchezaji mwandamizi wa klabu Jonas Gerrard Mkude.

 Lakini moja ya mambo yaliyo nifurahisha ni pale Mkude alipoongea kuwa hata yeye alipopewa kuna mchezaji alivuliwa hivyo amechukulia kawaida kwake. Tukio la mabadiliko ya kiuongozi sio geni Kwa wachezaji wanaojitambua. Hapa kwetu ilionekana tofauti sana kimapokeo. Wako waliofikiria mbali zaidi na kutaka kuuaminisha umma kuwa ni maajabu ya dunia.

 Hii ni kutokana na kutokuwa wafuatiliaji wa karibu wa mambo yanayoendelea katika vilabu vidogo nchini au nje ya nchi. Wakati watu walikichukulia suala la unahodha wa Bocco kama ni maajabu walisahau kama Yusuph Ndikumana wa Mbao aliposainiwa na klabu akapewa na unahodha.

 Ilikuwa ni maamuzi ya benchi la ufundi likiongozwa na Etienne Ndayigiragije kama kocha mkuu. Iliwahi tokea wakati Klabu ya Mbeya City imesainisha Juma Nyosso. Alipewa unahodha na kumfanya Hassan Mwasapili kuwa msaidizi wake. Sasa katika msimu huu ilikuwa ajabu Kwa Bocco ila Kwa Asante kwasi imeonekana kawaida.

 Hapo ndipo unapopata jawabu la kuteswa na ushabiki wa Simba na Yanga. Kila upande huona wafanyacho wenzao kina walakini. Mara baada ya kutambulishwa kama mchezaji wao,klabu ya Aston Villa ikamtangaza John Terry kuwa nahodha wao. Na hakuna aliyetilia shaka na maisha yameendelea. Ilikuwa pia Mara tu baada ya kusainishwa na klabu ya West Bromwich Albion,Darren Fletcher alipewa unahodha katika klabu hiyo.

 Wako wachezaji ambao ukiwa nao katika klabu wanakuwa na nyota pia wanakua na hali ya kiuongozi. Unapompa Unahodha Nyosso au Kwasi maanake unamfanya awaongoze wenzake kucheza kama yeye anavyocheza Kwa kujitoa. Hadi kufikia hatua mtu anapewa unahodha manake benchi la ufundi limepima mambo mengi ya faida toka Kwa mchezaji husika. 

Uongozi ni karama ili uongoze unahitaji kuwa na ari na mvuto wa kiuongozi Kwa wenzako. Nani anaweza kutia shaka juu ya Asante Kwasi. Ifike wakati tusijone kama sisi kila siku tunaosea kutokana na kutokufanya kama akina Fulani. 

Tunapaswa kuonyesha kile tunachokiamini na sio kuiga ili kuwafurahisha watu wengine. Kuwafurahisha watu ni kama kumchukua mchezaji kipenzi cha mashabiki na kumpa unahodha kitu ambacho pengine kikawa tofauti na matarajio ya wengi na kuonekana hajui kuongoza. 

Nafasi ya unahodha ni kubwa unahitaji watu wenye mvuto Kwa wachezaji wenzao na sio mashabiki. Unaweza kupendwa na mashabiki lakini ukawa huna ushawishi Kwa wenzako mkiwa vyumba vya kubadilishia nguo. Kiuongozi siku zote anakuwa mtu wa mfano katika kutenda na sio anasukumwa kutenda.

 Licha ya kuwa na kipaji kikubwa cha kucheza soka lakini Ronaldinho Gaucho hakuwahi kuwa nahodha Barcelona na hata Brazil. Akili ya kumchagua mchezaji kuwa kiuongozi hakumaanishi una kiwango bora kuliko wenzako hapana ila una muono mkubwa wa kiuongozi katika mpira Kwa wachezaji wenzako. Unahodha kwasi hautii shaka Kwa watu kwasababu ni lipuli au ilivyowahi kutotia shaka ule wa Nyosso na Mbeya city. 

Ukitaka kuona unahodha unajadiliwa na kuonekana ni kitengo nyeti Kwa watu maalumu usikie kuwa Yanga wamemteua Youthe Rostand kuwa nahodha. Mashabiki wao watakuja na hoja ya kutaka kujua kigezo kilichotumika kupewa unahodha. Wakati wale wapinzani wao watakuwa wanaona kama ajabu sana jambo hilo kutokea. Hivyo usishangae kusikia ikasemekana kuwa ni rekodi ya dunia. 

Hii ni kwasababu tu ya fikra za wengi kuishia katika kufuatilia soka na wachezaji wa Simba na Yanga. Kocha wa Lipuli Seleman Matola alitazama mengi toka Kwa mtangulizi wa Asante. Wakati wakiwa daraja la kwanza walikuwa na nahodha Ramadhani Kudunda na baadae Salumu Machaku ambaye hadi timu inapanda ligi kuu yeye ndo alikuwa nahodha. 

Lakini unapokuwa na mtu wa aina ya Asante Kwasi lazima umtumie vyema Kwa manufa ya klabu. Binafsi sikuona maajabu kama wakivyosema baadhi ya wadau kwasababu ya rejea zilizokuwepo juu ya nafasi ya Nahodha Kwa vilabu vingi duniani.

 Hivyo suala la Bocco haikuwa 'story' kama ilivyochukuliwa. Hii ni kama ilivyotokea Kwa Ndikumana,Terry,Nyosso,Fletcher na wengine ambao waliwasili katika klabu na kupata unahodha kama ilivyo Kwa Kwasi. Ifike wakati tuache weledi utumike vyema katika kujadili au kutolea ufafanuzi mambo yanayohusu utaalamu Fulani.

Tusizidiwe na maarifa kwasababu ya mapenzi na tukashindwa kung'amua Yale yanayohitaji akili.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad