HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 12, 2017

TRA yavuka lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka 2016/17

Mamlaka ya Mapato Tanzania imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi Trilioni 14.4 kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Makusanyo haya ni sawa na ukuaji wa asilimia 7.67 ikilinganishwa na makusanyo ya mwaka 2015/16 ambayo yalikuwa ni kiasi cha Shilingi Trilioni 13.3.

Sambamba na Makusanyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa kodi TRA Bw. Richard Kayombo alisema Mamlaka imeendelea kukusanya kodi mbalimbali ikiwemo kodi ya majengo na muitikio wake umekuwa ni wa kiwango cha kuridhisha.

Mamlaka inapenda kuwashukuru walipakodi wote kwa muitikio huo na wengine wanaoendelea kujitokeza katika ofisi mbalimbali za Mamlaka nchi nzima ili kuweza kulipa kodi hiyo ambayo mwisho wa kulipa kodi hiyo ni tarehe 15 Julai, 2017.

Aidha, Mamlaka inapenda kutoa wito kwa wafanyabiashara wote kutoa risiti za EFD pindi wanapouza bidhaa au huduma na Wananchi wote kuhakikisha wanadai risiti pindi wanaponunua bidhaa au kupata huduma na kuwa, kinyume na hapo watakuwa wanatenda kosa kwa mujibu wa sheria ya usimamizi wa kodi.

Hivi sasa kuna zoezi la uhamasishaji na ukaguzi linaloendelea nchi nzima katika sehemu zote za biashara kukagua wafanyabiashara wasiotumia Mashine za Risiti za Kielektroniki za EFDs pamoja na wananchi wote wasiodai risiti baada ya kununua bidhaa au huduma.

 “Napenda kuwakumbusha wananchi wote kuhakiki risiti zao ili kuona usahihi wa tarehe na kiasi walicholipa kabla ya kuondoka na risiti hiyo” alisistiza Kayombo

 ‘Pamoja Tunajenga Taifa Letu’

Richard Kayombo

MKURUGENZI WA HUDUMA NA ELIMU KWA MLIPAKODI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad