HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 14 July 2017

SERIKALI YAENDELEA KUBORESHA MFUMO WA HCIMS ILI UWEZE KUTUMIKA NA WATUMISHI WENGI ZAIDI

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akizungumza na viongozi na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe (hawapo pichani) leo alipofanya ziara ya kikazi  katika Kata hiyo ili kupokea maoni, ushauri na kusikiliza kero za watumishi wa umma Jijini Dar es Salaam. 
 Mhudumu wa Afya kutoka Hospitali ya Magomeni Bi. Rukia Mkapa akitoa malalamiko yake wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa kikao kazi na watumishi wa Kata ya Kawe kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
Mwalimu Paschal Mugayana kutoka shule ya Sekondari ya Njechele  akitoa malalamiko yake wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa kikao kazi na watumishi wa umma wa Kata ya Kawe kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.
 Sehemu ya watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) wakati wa kikao kazi na watumishi hao kilichofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora inaendelea kusanifu na kuboresha Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCIMS) ili uweze kutumika kutoa taarifa za msingi kwa watumishi  wa umma wengi zaidi kwa lengo la kuleta mabadiliko ya utendaji kazi katika sekta ya umma nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) amesema hayo leo katika kikao kazi na Watumishi wa Umma wa Halmashauri ya Manispaa ya  Kinondoni – Kata ya Kawe, jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kairuki amesema Mfumo wa HCIMS awali ulikuwa unapatikana Ofisi ya Rais–Utumishi pekee, lakini baadae ukakasimishwa kwa Maafisa Utumishi lakini sasa lengo ni kuwafikia watumishi wa umma waweze kuona taarifa zao ili kupata taarifa sahihi na za uhakika katika kanzidata. Amesema Tovuti ya Watumishi, Watumishi Portal, imeanzishwa maalum ili watumishi wa umma wajisajili kupitia tovuti ya Ofisi ya Rais-Utumishi yenye anuani www.utumishi.go.tz na kuona taarifa zao za msingi.
Waziri Kairuki, pamoja na hilo, amesema mfumo wa HCIMS umegatuliwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa hivi sasa ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kufanya maamuzi kwa haraka zaidi.
 “Kwa kuwa mahitaji ya watumishi wa umma ni mengi hivyo tumeona ni vema tukakasimu Mfumo huu na kwa watumishi wa umma katika kada nyingine ili kurahisisha utendaji kazi na kuleta mabadiliko” Mhe. Kairuki amesema.
Waziri Kairuki ameongeza kuwa tayari mafunzo kuhusu namna ya kutumia mfumo yalikwishatolewa kwa Maafisa Elimu na Makatibu wa Afya wapatao 633.
 “Tumeamua kuanza na sekta hizi kwa sababu ni sekta zenye watumishi wa umma wengi zaidi ukilinganisha na sekta nyingine lakini tutaendelea kugatua mfumo wa HCIMS ili ufike katika sehemu nyingi zaidi za kutolea huduma (Service Delivery Points).” Mhe. Kairuki ameongeza.
Mhe, Kairuki yuko katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Dar es Salaam, ambapo leo ni siku yake ya tano aliyoitumia kukutana na Watendaji na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni-Kata ya Kawe.
Lengo la ziara ni kukutana na watumishi wa umma na kusikiliza malalamiko, ushauri na changamoto zinazowakabili katika maeneo yao ya kazi ili kuweza kuzifanyia kazi na kuleta mabadiliko katika Utumishi wa Umma nchini. 

IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI
OFISI YA RAIS-UTUMISHI
14.07.2017

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad