HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, June 28, 2017

TAKUKURU YAENDELEA KUWASHIKILIA RAIS WA TFF MALINZI NA KATIBU WAKE MWESIGWA

Rais wa TFF Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake Selestine Mwesigwa.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imethibitisha kuwashikilia Rais wa TFF Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wake Selestine Mwesigwa kwa mahojiano.

Afisa uhusiano wa TAKUKURU Musa Misalaba amesema, ni kweli wanawashikilia viongozi wa TFF kwa ajili ya mahojiano ambapo wamekuwa wakifanya uchunguzi kwa muda mrefu kabla ya kuamua kuwashikilia kwa ajili ya mahojiano.

“Ni kweli kwamba tunaendelea na uchunguzi dhidi ya viongozi mbalimbali wa TFF na uchunguzi huo tumekuwa nao kwa muda mrefu lakini kuhusu kuwashikilia kwa nini, bado ni siri yetu upande wa uchunguzi, katika uchunguzi tunaongozwa na misingi ya sheria, kanuni na taratibu hatuwezi tukaweka wazi kila jambo.”

Misalaba amesema kuwa Jambo la msingi ambalo wananchi wanatakiwa kuelewa ni kwamba, kuna uchunguzi ambao wanaendelea nao ambao umekuwa ukifanywa kwa muda mrefu na kuhusiana kuwashikilia Malinzi na Mwesigwa wamesema muda wa uchunguzi ukikamilika watawapeleka mahakamani.

“Tunawashikilia na bado tuko nao chini ya ulinzi wetu , tunaongozwa na sheria tutakapomaliza uchunguzi wetu tutaweka wazi kama ni kuwaachia ila ushahidi ndio utakaoamua lakini ni lini ni swala kiuchiunguzi, lakini ni siri ya uchunguzi.”

Hivi karibuni gazeti la Nipashe liliandika mfululizo wa makala zilizokuwa zikielezea tuhuma za ufisadi zilielekezwa kwa Malinzi na viongozi wenzake wa TFF.

JAMALI AMEFANYA HAYA UFISADI WA KUTISHA TFF

Ripoti ya ukaguzi wa fedha za udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania kwa Taifa Stars iliyotolewa Oktoba 2, 2014, inaelezwa kuwa, mbali na mambo mengine, TBL iliamua kufanya ukaguzi huo ili kujiridhisha kama shirikisho linazingatia makubaliano yaliyomo kwenye mkataba.

Inaelezwa katika ripoti hiyo ambayo uongozi wa juu wa TBL uliithibitishia Nipashe jana kwamba ilifanywa na Mkaguzi Mkuu wake wa ndani, Richard Magongo, kuwa kati ya Novemba 13, 2013 (siku 11 tangu uongozi wa sasa wa TFF uingie madarakani) na Februari 15, 2014, Dola za Marekani 315,577 (Sh. milioni 688.368) zilitumika bila ya nyaraka za kuthibitisha matumizi yake kinyume cha makubaliano ya mkataba wa pande hizo mbili.

Kati ya Novemba 11, 2013 na Machi 11, 2014, Dola za Marekani 381,248 (Sh. milioni 831.616) pia zilichotwa kwenye akaunti hiyo na kutumika kwa shughuli ambazo hazijaanishwa katika mkataba wa TBL na TFF, ripoti inabainisha.

Mchanganuo wa ripoti hiyo unaonesha kuwa, miongoni mwa waliotajwa kwenye ripoti hiyo kutumia fedha hiyo ni pamoja na rais wa TFF, Jamal Malinzi, ambaye Desemba 24, 2013 alilipwa Dola za Marekani 159 kupitia vocha yenye namba 1075 zikiwa ni gharama za malazi hotelini (Hotel accommodation).

Ripoti inaonesha kuwa, siku hiyo hiyo (Desemba 24, 2013), Malinzi alilipwa na TFF Dola 10,000 kupitia vocha namba 1077 (Repayment to Jamal Malinzi/Marejesho ya fedha za Jamal Malinzi), kisha Februari 6, 2014 akalipwa Dola 15,934 (Loan Repayment to Jamal Malinzi/Marejesho ya mkopo kutoka kwa Jamal Malinzi) na baadaye kulipwa Dola 69,471 kupitia vocha namba 1098 na Dola 63,735 kupitia vocha namba 1401.

Wengine waliopewa fedha hiyo ya udhamini wa TBL kwa Taifa Stars ni aliyekuwa msaidizi wa Malinzi, Juma Matandika, Ali Ruvu na mwingine aliyetajwa kwa jina la S. Madadi ambao kwa pamoja walilipwa Dola 1,084 kupitia vocha namba 828 Februari 6, 2014.

Ripoti pia inabainisha malipo ya Dola 3,500 Januari 16, 2014 kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF jijini Nairobi.

Pia zimo Dola 4,630 zilizochotwa Desemba 24, 2013 kugharamia mtihani wa utimamu wa mwili kwa waamuzi (Cooper test for referees), Dola 4,120 zilizotolewa siku hiyo hiyo kwa ajili ya Ally Mayay na Ayubu Nyenzi kufanya ziara Uganda na Dola 1,638 ambazo zilitolewa siku hiyo hiyo zikiwa fidia ya malipo ya deni la TFF kulipia ziara ya uongozi wa shirikisho mkoani Mwanza.

Dola 4,023 zilitolewa Desemba 24, 2013 kwa ajili ya posho ya sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya kwa wafanyakazi wa TFF na Dola 30,000 zilitumika kwa semina elekezi kwa makocha iliyofanyika Lushoto (coach retreat at Lushoto), ripoti inasema.

Inaongeza: “Dola 2,829 zilitumika kutoa rambirambi na misaada, Dola 3,298 zikakopeshwa kwa Chama cha Soka Mbeya huku Dola 989 zikitolewa kwa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara zikiwa ni msaada.”

Katika ripoti hiyo, inaelezwa kuwa, Dola 90,000 zilitumika kulipia fidia ya kuvunjwa kwa mkataba wa aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na Dola 34,177 zikatumika kununua magari mawili aina ya Toyota Hiace.

Ripoti inaeleza kuwa, kulikuwa na mawasiliano rasmi kati ya maofisa wa TFF na TBL kabla ya kufanya malipo kwa Poulsen na ununuzi wa magari hayo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad