HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 18 June 2017

PROGRAMU YA KUKUZA UJUZI MWAROBAINI WA TATIZO LA AJIRA KWA VIJANA

Na Ismail Ngayonga, MAELEZO

TAKWIMU za  Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonesha kuwa idadi ya vijana nchini wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ni takribani Milioni 16.2 sawa na asilimia 35.1 ya Watanzania wote.

Aidha, Utafiti wa Nguvu Kazi wa mwaka 2014 unaonesha kuwa vijana ni asilimia 59 ya nguvu kazi ya Taifa, ambapo asilimia 16.6 pekee ndio wenye kiwango cha ujuzi wa kati katika kujiajiri au kuajiriwa.

Matokeo ya tafiti hizo yanathibitisha kuwa kuna umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana na ushirikishwaji wao katika mipango ya maendeleo ikiwemo uanzishaji na utekelezaji wa programu maalum za kukuza ujuzi na maarifa kwa kundi hilo.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi Nchini (2015/2016–2019/2020) iliyokusudia kuwezesha nguvu kazi ya Taifa kupata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Utekelezaji wa programu hiyo ni hatua za makusudi za Serikali za kukabiliana na kiwango kidogo cha ujuzi miongoni mwa nguvu kazi inayohitajika kuongeza idadi ya watu wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia 3 ya sasa hadi asilimia 12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda.

Aidha Programu hiyo inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekusudia kuziba pengo kubwa lililopo la ukosefu wa ujuzi stahiki katika sekta za utalii na ukarimu, ujenzi, viwanda, nishati na madini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Ajira katika Ofisi ya Waziri, Bw. Robert Masingiri anasema Programu ya kukuza ujuzi nchini imetokana na majadiliano kati ya Waajiri/ Sekta Binafsi na Serikali kupitia Kamati Elekezi ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) inayosimamia eneo la Sheria za Kazi na Ukuzaji Ujuzi tozo.

Masingiri anasema Programu hiyo pia imekusudia kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa Wafanyakazi vijana 13,400 waliopo makazini ili kuweza kurasimisha ujuzi wao na kuwawezesha kushriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Anasema katika kutekeleza Programu hiyo, katika mwaka wa fedha 2015/16 Serikali ilitenga kiasi cha Tsh. Bilioni 15 na takribani vijana 500 wamehitimu mafunzo ya ujuzi wa utengenezaji nguo na kuajiriwa katika kiwanda cha nguo cha Tanzania TOOKU Garment Company Ltd.

Masingiri anaongeza kuwa Serikali pia imeingia mkataba na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa ajili ya kurasimisha ujuzi wa vijana 3900 katika fani za ujenzi, uashi na useremala.

“Tunatarajia kutoa mafunzo ya kujenga uwezo kwa warasimishaji 150 katika kanda ya kati ya VETA yenye mikoa ya Dodoma, Singida na Manyara, Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Tanga na Kilimanjaro, Kanda ya magharibi yenye mikoa ya Shinyanga, Kigoma na Tabora” anasema Masingiri.

Aidha Masingiri anasema hadi kufikia Serikali pia imeandaa na kukamilisha  Mwongozo wa Kitaifa wa kutoa mafunzo kwa vitendo kupitia Uanagenzi na kuandaa Mwongozo wa Kitaifa wa kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu.

Anaongeza kuwa Serikali pia imefanikiwa kuhuisha Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008 na kukamilisha rasimu ya awali ili kuwawezesha vijana wengi kuajirika na kujiajiri, na kuweza kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.

Moja ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira kwa vijana ni kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika, hivyo utekelezaji wa Programu hiyo utasaidia kupunguza pengo la mahitaji ya rasilimali watu nchini ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya haraka ya uchumi wa viwanda.

Kwa kutambua kuwa Vijana ni hazina na rasimali watu muhimu kwa maendeleo ya Taifa, Serikali imewawezesha vijana kiuchumi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo hadi kufikia mwezi Machi 2016 kiasi cha Tsh. Bilioni 1.6 zilitolewa kwa kwa vikundi vya vijana 284.

Aidha kupitia mfuko pia pia Serikali imeweza kutoa mafunzo kwa viongozi wa vikundi 2,552 kutoka Halmashauri 59 pamoja na kutenga maeneo maalum ya shughuli za kiuchumi na huduma kwa vijana katika Halmashauri 30 nchini.

Ni wajibu wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha ukuzaji wa ajira unakuwa ni agenda ya msingi ya kudumu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad