HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, June 2, 2017

DC Simanjiro atatua mgogoro wa ardhi kata ya Terrat

Wakazi wa Kijiji cha Terrat Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Zephania Chaula, aliyeutatua mgogoro wa ardhi wa wakulima na wafugaji wa eneo hilo.

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Zephania Chaula, amefanikiwa kutatua mgogoro wa ardhi uliokuwa unafukuta kwenye Kata ya Terrat, kwa kupiga marufuku matumizi mengine ya sehemu ya kulishia mifugo na wanyamapori.

Akizungumza kwenye mkutano wa wananchi wa eneo hilo, Chaula ameuagiza uongozi wa Kijiji cha Terrat kupima eneo lote lililotengwa kwa ajili ya mifugo na wanyamapori na mipaka yake ibainishwe.

Pia, ametoa miezi miwili kwa wakulima waliovamia na kulima sehemu ya eneo hilo kuondoka kwa hiyari yao wenyewe ifikapo Julai 31 mwaka huu na endapo watakaidi agizo hilo wataondolewa kwa nguvu.

Alisema eneo la kingo ya mifugo libainishwe ukubwa wake na pia mipaka yake ipimwe baina ya vijiji vya Terrat na Loiborsiret ili kuondokana na sintofahamu ya mwishilio wa eneo hilo.

Alisema serikali ya kijiji ibainishe maeneo ya wazi yaliyowekwa kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi na kuonyesha maeneo ya kilimo na mifugo na kutolewa mapendekezo kupitia mikutano ya kijiji.

“Pamoja na hayo nahitaji hadi Juni 15 mwaka huu, niletewe taarifa juu ya uvamizi wa watu watano ambao wanalima kwenye sehemu hiyo ambayo wananchi wa Terrat wanailalamikia,” alisema Chaula.

Alisema serikali ya kijiji hicho pia, iangalie namna ya kukutana na watu 527 wa Terrat ambao wana mgogoro wa ardhi wakidaiwa kuinga kwenye sehemu ya malisho na kutumia eneo hilo kwa kilimo.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo Yefred Myenzi alisema ardhi ni mali ya wananchi wote na endapo kutatokea mgogoro wa ardhi sheria ya ardhi inaagiza namna ya kuutatua.

Myenzi alisema kupitia sheria hiyo wamefanya jitihada ya kupata suhulu juu ya mgogoro wa kijiji cha Terrat na Loiborsiret na atatoa taarifa kwa mkuu wa wilaya hiyo ifikapo Juni 15 mwaka huu.

“Kunapotokea mgogoro wa ardhi tunafanya jitihada na kuhakikisha unamalizika hivyo wale watu 25 wanahitajiwa wahudumiwe na upande wa Terrat na wale wengine wakahudumiwe kule,” alisema.

Diwani wa Kata ya Terrat Jackson Materi alipongeza jitihada za mkuu wa wilaya hiyo kuhakikisha anamaliza mgogoro huo ambao ulitaka kusababisha mpasuko na mshikamano wa wananchi wa eneo hilo.

“Pamoja na hayo bado tutaendelea kuwa pamoja na wananchi wangu na nilishawaeleza tangu hapo awali kuwa mimi sina ardhi hivo matumizi ya ardhi yenu mtajipangia ninyi wenyewe,” alisema Materi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad