HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 15 May 2017

Wabunge wageuzwa ATM kwa kujitakia

Wakati wabunge wakionyesha kukerwa na kugeuzwa ATM majimboni kwao, Katibu wa Spika, Saidi Yakubu amewaeleza kuwa wao ndio chanzo hivyo wakiamua tatizo hilo litakwisha.
Yakubu alikuwa akijibu hoja mbalimbali za wabunge zilizotolewa walipokuwa wakichangia kwenye semina kuhusu wajibu wa wabunge wanachama wa mabunge ya nchi za Jumuiya ya Madola (CPA) katika kufanikisha maendeleo endelevu.
Alisema wabunge wamekuwa ni sehemu ya tatizo hilo kwani mwaka 2008 waliendesha mradi wa kutoa elimu kwa umma na walikwenda katika mikoa mbalimbali ikiwamo Ruvuma lengo likiwa ni kuwaeleza majukumu ya mbunge kwa wapigakura.
“Tuliwaeleza wananchi kuwa kazi ya mbunge sio kulipa ada, bali ni kushawishi Serikali kuangalia upya ada kama gharama ni kubwa,” alisema.
Hata hivyo, alisema baada ya maelezo hayo alisimama diwani mmoja na kusema mtoa mada amewadanganya mbona mbunge (aliyekuwapo eneo hilo) alimuahidi kuwa akishinda ubunge atampatia fedha.
Alisema tabia ya wabunge kutoa fedha kwa wananchi sio kwa Tanzania tu, bali imejitokeza kwa nchi nyingine ikiwamo India, Australia (baadhi ya maeneo) na kuwashauri kuungana kulimaliza tatizo hilo.
Katibu huyo alisema wabunge wana jukumu la kulitatua tatizo hilo kwa sababu fedha wanazopata ni ndogo na hawawezi kutoa kwa mtu mmoja mmoja.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alisema katika nchi mbalimbali ikiwamo Kenya ofisi ya mbunge ni taasisi tofauti na Tanzania ambapo mbunge ni ATM. “Mbunge wa Tanzania ni ATM, ni kabenki kadogo pamoja na ufinyu wa fedha anazopata lakini kila mwezi anakatwa Sh1.2 milioni na mafao yake ya mwisho (baada ya miaka mitano) pia anakatwa, ukiagiza gari pia unakatwa,” alisema.
Alisema kukiwa na harambee mbunge anaitwa kama mgeni rasmi na kutakiwa kuchangia wakati mwingine Sh70 milioni na kuhoji fedha hizo zinatoka wapi.
Akizungumzia demokrasia na uhuru wa mawazo, Waitara alisema utakuta mbunge ana jambo zuri lakini anashindwa kulizungumzia kwa sababu ya itikadi ya vyama.
Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugola alisema Tume ya Utumishi wa Bunge imelifanyia kazi suala la bima ya maisha ya afya kwa wabunge ambalo lipo kisheria lakini hawajahi kupata haki hiyo.
Alisema Tume ya Utumishi wa Bunge imuite Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kumwelezea kuhusu jambo hilo ambalo liko kisheria lakini hakulifanyia kazi.
“Wabunge hawana bima ya maisha ya afya ingawa ipo kisheria na wengi wamekufa na kupata ulemavu,” alisema.
Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghenjwa Kaboyoka alisema kamati za za Bunge hazina ofisi ambazo zinawawezesha kukaa na kupanga mipango yao. Pia alisema wabunge wameendelea kuchangia kichama na hivyo kushindwa kuitikisa Serikali hata kama wakiwa na msimamo katika jambo lenye masilahi kwa wananchi.
Mbunge wa Songwe (CCM) Philipo Mulugo alitaka mchanganuo wa mishahara, marupurupu na posho ya jinsi yanavyolipwa mabunge mengine ya Jumuiya ya Madola ili walinganishe na ya kwao.
Akijibu hoja za wabunge, Yakubu alisema nia yake ilikuwa ni kuchokoza mada lakini utafiti wa mafao umefanyika katika mabunge ya jumuia hiyo na kwamba kuupata hapo walipo ni ngumu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad