HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, May 30, 2017

SIKU YA MAZINGIRA DUNIANI: Elimu zaidi inahitajika kuhifadhi mazingira nchini

WAKATI Mataifa mbalimbali yanaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani yanayofikia kilele chake hapo Juni 5, 2017, takriban hekta 372,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini Tanzania kutokana na shughuli mbalimbali. Mwandishi Beatrice Lyimo wa Idara ya Habari - MAELEZO anaelezea zaidi.

Kwa miaka mingi siku ya Mazingira duniani imekuwa ikiadhimishwa kwa Wadau katika nchi mbalimbali kuchukua hatua chanya zinazohusu mazingira. Siku hii pia imekuwa ni sehemu ya kampeni ya utoaji elimu juu ya maswala yanayojitokeza kuhusiana na mazingira.

Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu inasema “Mahusiano Endelevu Kati ya Binadamu na Mazingira” ikihamasisha jamii kuwa na urafiki endelevu na mazingira asilia ambapo kila mtu anapaswa kutambua, kufurahi, kujivunia na kulinda uzuri wa mazingira asilia na kuhamasishana ili kuyatunza na kuyahifadhi.

Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingi Barani Afrika na duniani kwa ujumla imeendelea kuathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa mazingira unaotokana na shughuli mbalimbali zikiwemo za kilimo, ufugaji, ujenzi n.k

Mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu aliagiza kutofanyika kwa maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika ambayo yalizoeleka na badala yake Watanzania waadhimishe siku hiyo kwa kufanya usafi.

Mtazamo wa wengi kuhusiana na maelekezo ya Dkt. Magufuli ulilenga zaidi katika kubana matumizi mabaya ya fedha za Serikali.  Pamoja na mtazamo huo Mhe. Rais aliona mbali zaidi, kwani usafi wa mazingira unasaidia kudhibiti milipuko ya magonjwa kama vile kipindupindu, ambayo yanaigharibu Serikali fedha nyingi zaidi ya zile ambazo zingetumika katika kufanikisha maadhimisho hayo.

Hivyo uamuzi alioutoa Mhe. Rais utakumbukwa zaidi wakati huu ambapo nchi mbalimbali zinaadhimisha Siku ya Mazingira Duniani. Siku hii inatutaka tutoke nje tuone mazingira yetu yalivyo, tuone thamani yake na tupaze sauti ya kuulinda ulimwengu tunamoishi.

Inakadiriwa takribani hekta 372,000 za misitu hupotea kila mwaka nchini kutokana na shughuli za kilimo na ufugaji kwa njia zisizo endelevu. Uharibifu huu wa misitu unachangia pia kukosekana kwa mvua, kukauka kwa mito, mabwawa na uoto wa asili.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Mazingira duniani mwaka jana Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kazi ya kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira inahitaji ushirikiano wa Wadau katika ngazi zote.
Amesema, Serikali inahitaji ushirkiano mkubwa kutoka kwa wananchi, Vyombo vya Vabari, Taasisi na Asasi za Kiraia katika kutekeleza kikamilifu Sheria na Kanuni za uhifadhi wa mazingira nchini ili kupunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira.

Aidha,  Makamu wa Rais alizitaka Mamlaka katika ngazi mbalimbali ziwe na Mipango bora ya ardhi, mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vya maji, pamoja na udhibiti wa uvunaji holela wa misitu na ufugaji usio endelevu. 

Mama Samia pia alizitaka Wizara na Taasisi zote za Serikali na zisizo za Kiserikali kuendelea kutoa elimu juu umuhimu wa kutunza mazingira na faida zinazopatikana ili Wananchi waunge mkono jitihada zinazofanywa katika kulinda na kuhifandhi mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

 “Usafi wa mazingira uhusishe kila mtu kuhakikisha taka zinakusanywa na zinatupwa katika maeneo yaliyotengwa na tupande miti mingi wakati wa msimu wa mvua ili tujihami na kuenea kwa hali ya jangwa na mabadiliko ya tabianchi” alisema Mhe. Samia.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka 2017/18, Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema kuwa uchumi wa Tanzania unategemea   kwa   kiasi   kikubwa   maliasili  zilizopo  ikiwemo ardhi,  maji,  misitu  na hewa safi.

Alisema, maliasili zilizopo  zinahitajika kwa matumizi ya vizazi vilivyopo na vijavyo, hivyo uwepo wake hutegemea zaidi uhifadhi wa rasilimali hizo na  matumizi katika jamii inayotuzunguka.

Aidha, Waziri Makamba alibainisha baadhi ya  Changamoto iliyopo kwa sasa ni pamoja na uelewa mdogo wa jamii kuhusu  uhifadhi  ya  mazingira  na  uwepo  wa  mabadiliko  ya  tabianchi. Hivyo juhudi kubwa inahitajika zaidi katika kutoa elimu kuhusiana na mazingira.

Kwa mujibu wa Waziri Makamba, Serikali imeanisha programu mbalimbali za uhifadhi mazingira kwa kutengeneza, kusimamia na kuhamasisha utekelezaji wa mipango na mikakati  ya Kitaifa ya hifadhi na usimamizi wa mazingira  nchini katika ngazi mbalimbali za utawala.

“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali iliwahimiza  viongozi na watendaji katika Sektretarieti za Mikoa,  Mamlaka za Serikali za Mitaa na Sekta zote Tanzania  Bara kutenga fedha na kutekeleza na kutolea taarifa  mikakati na mipango ya hifadhi na usimamizi wa  mazingira” alisema Mhe. Makamba.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais TAMISEMI iliandaa Mkakati wa Taifa wa  Kupanda na Kutunza Miti  utakaotekelezwa  kwa  kipindi cha miaka mitano (2016 hadi 2021) ambapo  mkakati  huo unaelekeza katika kila kijiji, kitongoji, mtaa na  kaya  . 

Amesema, Mkakati huo umezingatia  kurekebisha changamoto zilizojitokeza katika  mikakati na kampeni zilizopita, ikiwemo motisha na ushiriki wa sekta binafsi katika biashara ya misitu ambapo baadhi ya mikoa imeanza utekelezaji wa mkakati huo kwa kupanda miti kwenye maeneo yao.

Tarehe 5 Juni kila mwaka Tanzania tunaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, ambapo kampeni mbalimbali huandaliwa kwa ajili ya kuhamasisha jamii kujenga uelewa wa masuala yahusuyo mazingira kuchukua hatua stahiki za kuhifadhi na kulinda mazingira.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad