HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 25 May 2017

SERIKALI YAWAHIMIZA WANANCHI KUCHANGAMKIA MIFUKO YA UWEZESHAJI KIUCHUMI NCHINI.

Na Daudi Manongi, MAELEZO DODOMA
Serikali kupitia Baraza la Uwezeshaji wananchi kiuchumi (NEEC) lililopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu imewataka wananchi kuitumia vyema mifuko 19 ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kujipatia mitaji yenye riba nafuu.
Hayo yamesemwa leo Bungeni na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Ajira na Vijana Mhe.Anthony Mavunde wakati akijibu maswali mbalimbali ya wabunge leo Mjini Dodoma.
“Serikali inawawezesha wananchi ili waweze kukopesheka kupitia Sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi Na.6 ya mwaka 2004, Alisema Mhe.Mavunde.
Amesema Sera hii imeainisha nia ya Serikali ya kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji kwa kuboresha vyanzo vya akiba na kuchukuwa hatua za kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwezesha mabenki kukopesha kikamilifu amana zilizopo kwa gharama nafuu,kupitia vikundi vidogo,SACCOS na Vicoba.
Aidha kutokana na Sera hii Mipango, Miradi na Mifuko kadhaa imeanzishwa na Serikali ili kuwezesha wananchi kukopa kwa urahisi ambapo katika mifuko hiyo 19 baadhi yake ni pamoja na Mfuko wa kuendeleza wajasirimali wananchi,mfuko wa
uwezeshaji wa mwananchi,mfuko wa pembejeo za kilimo,mfuko wa maendeleo ya
vijana, mfuko wa dhamana za mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati,mfuko wa
dhamana za mikopo kwa mauzo ya nje ya nchi ambapo hadi kufikia mwaka 2016 mifuko hii ilikuwa imetoa mikopo ya trilioni 1.7 kwa wajasiriamali 400,000.
Pamoja na hayo Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri kwa vyombo hivyo kuweza kutoa huduma kwa wananchi.
“Serikali kupitia Benki kuu ya Tanzania kulingana na mazingira inaendelea kuangalia viwango vya riba kwa mabenki na Taasisi za fedha ili zimudu kupata fedha zaidi kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali kwa riba ndogo,ambapo pia imechukua hatua ya kupunguza kiwango cha riba kwa mikopo yake kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12 ”,Alisisitiza Mavunde.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad