HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 26 May 2017

KITUO CHA AFYA UWEMBA CHAPATA CHUMBA CHA UPASUAJI, WALIA NA UKOSEFU WA JOKOFU LA DAMU NA JENERATOR

Hyasinta Kissima-Njombe
Miongoni mwa changamoto zinazoikumba sekta ya afya hususani katika maeneo ya pembezoni mwa Miji ni ukosefu wa huduma bora za afya na za kisasa pamoja na ukosefu wa vifaa tiba.

Katika Halmashauri ya Mji Njombe Kituo cha afya cha Mtakatifu Anna kinachomilikiwa na shirika la masista wa Benedictine kilichopo Uwemba, takribani KM 30 kutoka yalipo makao makuu ya Halmashauri ni miongoni mwa vituo vya afya 08 katika Halmashauri vinavyotoa huduma za afya kwa zaidi ya Kata 5 zinazoizunguka Halmashauri ya Mji Njombe.

Miongoni mwa changamoto iliyokua inakikabili kituo cha Mtakatifu Anna Uwemba tangu mwaka 1997 ambapo kilipandishwa hadhi na kuwa kituo cha afya ni ukosefu wa chumba cha Upasuaji. Wazo la uanzishaji wa chumba cha upasuaji lilianza mwaka 2008 na kufikia 2013 kituo hicho kilipata ufadhili kutoka Uholanzi kupitia Mfadhili wao Monique Derrez na Leon Van ambao wao walijitolea kuhakikisha ujenzi na utoaji wa vifaa vya kisasa katika  chumba cha upasuaji.
Akizungumza wakati wa ibada ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha ujenzi wa Chumba hicho cha upasuaji Kaimu Naibu Askofu Jimbo Katoliki la Njombe Padre Exavery Mlelwa amesema kuwa ni jambo la heri kumshukuru Mungu kwa Ujenzi wa chumba hicho lakini pia kuwashukuru na kuwaombea Wamisionari waliotangulia na kuanzisha huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchi ambazo leo hii huduma hizo zimekuwa ni za msaada kwa jamii ya Watanzani wote na amewasisitiza wazazi kuhakikisha wanawasomesha watoto wao ili kuweza  kupata wataalamu wazuri zaidi katika sekta ya afya kwa siku za mbeleni.

“Ni vyema kuuenzi uhai tuliojaliwa na mwenyezi Mungu kwa kulinda afya zetu, kufanya vipimo lakini pia kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wetu wa afya na kufuata maelekezo ya madaktari. Uwepo wa Chumba cha Upasuaji Uwemba ni habari njema ya kuimarisha huduma ya afya. Hivyo ni jukumu letu kuhakikisha huduma zinaendelezwa kwa kuhakikisha mnasomesha watoto na kutoa ulinzi wa kutosha kwa kulinda kituo chetu cha afya ili kiweze kuwa na manufaa vizazi na vizazi.” Alisema.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe Gualbert Mbujilo akikata Utepe Kuashiria Uzinduzi wa chumba cha upasuaji.Nyuma yake ni Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Njombe Dkt. Samwel Thomas Ndalio

Akionesha hali halisi ya vifo vinavyosababishwa na ukosefu wa huduma za upasuaji kwa kina mama Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Njombe Dkt. Samwel Thomas amesema kuwa idadi ya watoto waliopoteza maisha kutokana na kuchelewa kupata huduma kwa kinamama wanaojifungua (Infant Death) kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Machi 2017 katika Halmashauri yake  ni vifo 37 vilivyoripotiwa ambapo kwa kiasi kikubwa vifo hivi vimesababishwa na ukosefu wa huduma za upasuaji katika maeneo jirani na amepongeza uzinduzi huo wa chumba cha upasuaji kwani itapunguza idadi ya kinamama wengi hususani wa maeneo ya Uwemba na Kata za jirani kusafiri hadi mijini kutafuta huduma za upasuaji jambo ambalo limekua likihatarisha maisha yao na watoto wanaozaliwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Gualbert Mbujilo, amesema kuwa Halmashauri kwa sasa inasubiri mifumo mipya ya mikataba kati ya Serikali na sekta binafsi juu ya uendeshaji wa vituo vya afya na ameahidi pindi itakapokuwa tayari Halmashauri itatoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha yale yaliopo kwa mujibu wa miongozo yanatekelezwa ipasavyo.

Muonekano wa ndani wa Chumba cha Upasuaji.

Wakati huo huo amewasisitiza viongozi wa Vijiji, Kata na Watendaji kuhakikisha wanawahamasisha Wananchi kujiunga na Mfumo wa afya CHF  kwani kwa kipindi cha mwaka mmoja familia itatibiwa kwa kiasi cha shilingi elfu kumi na hii itasaidia si tuu upande wa familia bali pia kupitia CHF kituo cha afya kitaweza kujiendesha kwa ufanisi zaidi.

Kwa sasa kituo hicho kinakabiliwa na ukosefu wa Jokofu la kuhifadhia damu, jenerator la dharura pindi umeme unapokatika ghafla na wameiomba serikali, makampuni binafsi  na watu wenye mapenzi mema  kuona ni jinsi gani inaweza kuwasaidia upatikanaji wa vifaa hivyo kwani kwa sasa vinaumuhimu mkubwa kutokana na uwepo wa chumba hicho cha upasuaji.
Sister Scholastika ni Daktari katika kituo hicho cha Afya akitoa ufafanuzi wa kazi za vifaa mbalimbali katika chumba cha upasuaji kwa wananchi waliohudhuria kwenye uzinduzi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad