HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 11 April 2017

VYAMA VYA USHIRIKA MANYARA KUNUNUA MAZAO YA WAKULIMA

Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini, Tito Bathelemeo Haule akizungumza mjini Babati Mkoani Manyara, kwenye jukwaa la vyama vya ushirika, lililojumuisha wanachama wa wilaya za Simanjiro, Kiteto, Mbulu, Hanang' na Babati.
 Ofisa elimu wa Mkoa wa Manyara, Arnold Msuya akifungua jukwaa la vyama vya ushirika la mkoa huo mjini Babati, kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Dr Joel Bendera.
 Mwanachama wa Hekima SACCOS ya Wilayani Hanang' Mkoani Manyara Jackson Mtesi akizungumza mjini Babati kwenye jukwaa la vyama vya ushirika vya mkoa huo.
 Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Manyara, Venance Msafiri akizungumza kwenye jukwaa hilo mjini Babati.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera amesema katika msimu huu wa kilimo, serikali kupitia bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko (CPB) itanunua mazao ya wakulima kwa kutoa bei nzuri inayokidhi bei ya soko.

Dk Bendera aliyasema hayo mjini Babati kwenye jukwaa la vyama vya ushirika vya mkoa huo ambapo hotuba yake ilisomwa kwa niaba yake na ofisa elimu wa mkoa huo Arnold Msuya.

Alisema watafanikisha zoezi hilo kupitia vyama vya msingi Amcos na chama kikuu Rivacu, kwa kuvitumia kama vituo vya kununulia mazao ya wakulima kwa bei itakayokidhi gharama za uzalishaji.

Alitoa rai kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika kutumia fursa hiyo vizuri kukusanya mazao kutoka kwa wakulima katika ubora unaostahili na kutojihusisha na vitendo vya ubadhirifu na wizi.

“Katika kueleka uchumi wa viwanda, vyama vya ushirika hususani AMCOS na RIVACU vina fursa kubwa kuchangia uchumi wa viwanda kwenye  mkoa huu kwani vinategemewa kuwa wazalishaji wa malighafi za viwanda vidogo vya kati na vikubwa,” alisema.

Mrajisi wa vyama vya ushirika nchini Tito Haule aliwataka mrajisi msaidizi wa ushirika wa mkoa huo na maofisa ushirika wa wilaya kuwajengea uwezo wanaushirika kupitia vikundi vyao.

“Wana ushirika wanatakiwa kila mara kupewa elimu ya ushirika na pia kukaguliwa mahesabu yao ili vikundi vyao viimarike na endapo mtashindwa hilo ninyi ndiyo mtakaobeba lawama,” alisema Haule. 

Mrajisi msaidizi wa ushirika wa mkoa huo, Venance Msafiri alisema Manyara ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa na vyama 93 hadi sasa wapo 246 na wana ushirika hao huweka hisa za sh1.1 bilioni, akiba ya sh3.4 bilioni na amana ya sh133.2 milioni.

Alisema kati ya idadi hiyo, vyama vya ushirika 104 vipo sinzia yaani havifanyi kazi ya kutoa huduma kama ilivyotarajiwa ila vyama vya ushirika vinaendelea kuimarika na kufanya kazi zao ipasavyo.

“Kuna chama kikuu cha ushirika kimoja cha Rivacu, kuna Saccos 150, vyama vya ushirikia vya mazao 67, mifugo 17, viwanda vidogo sita, madini vitatu, taasisi mbili na duka moja” alisema Msafiri.

Alisema mitaji ya Saccos siyo mikubwa kutokana na viwango vidogo vya hisa, akiba, amana na viingilio vidogo, ila ili kuhakikisha vyama hivyo vinaimarika wana hamasisha viungane ili viwe na nguvu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad