HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 15, 2017

MIILI YA ASKARI NANE WALIOUAWA MKOANI PWANI YAAGWA JIJINI DAR, WAZIRI MWIGULU ATANGAZA KIAMA KWA WATUHUMIWA

Na Dotto Mwaibale 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba amewatangazia kiama watu wote waliohusika kuwaua askari polisi nane Kibiti wilayani Mkuranga mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa kuaga miili ya askari hao jijini Dar es Salaam leo asubuhi Mwigulu alisema watu hao watakamatwa wote na kufikishwa kwenye mkono wa sheria. "Kitendo hiki cha mauaji kilichofanyika dhidi ya askari wetu hakivumiliki hata kidogo waliohusika tutawatafuta na kuwakamata" alisema Mwigulu.

Aliwaomba wananchi wa maeneo husika kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwapata wahusika wa tukio hilo. Katika hatua nyingine Mwigulu ameitaka wizara husika kuhakikisha inatoa fidia kwa ndugu wa askari hao na majeruhi badala ya kuchukua muda mrefu kuitoa. "Naomba fidia kwa askari hawa tuliowapoteza wakitumikia taifa itolewa haraka bila kucheleweshwa" aliongeza Mwigulu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu alisema watuhumiwa wote waliohusika kufanya mauaji hayo ni lazima watafikiwa na mkono wa dola. Alisema wananchi wa eneo hilo wanawafahamu wahusika hivyo amewaomba washirikiane na polisi ili kuwapata vinginevyo nguvu itatumika.

Alisema linapotokea tukio kama hilo kuna baadhi ya watu wamekuwa wakishabikia kupitia mitandao ya kijamii hivyo akatoa onyo kuwa watakao bainika na wao watakamatwa kwa kutenda kosa.

Askari waliopoteza maisha katika tukio hilo la kinyama wametajwa kuwa ni pamoja na Mkaguzi Msaidizi Peter Kiguu, Koplo Francis, PC Haruna, PC Jackson, PC Zakaria, PC Siwale, PC Maswi na PC Ayoub.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini, Mwigulu Nchemba, akitoa heshima za mwisho Dar es Salaam leo mbele ya majeneza yenye miili ya askari nane waliouawa na majambazi Kibiti wilayani Mkuranga mkoani Pwani juzi jioni.Kulia kwake ni Naibu Waziri wa wizara hiyo, Hamad Masauni.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini, Mwigulu Nchemba, akitoa pole kwa wafiwa.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchini, Mwigulu Nchemba (kulia), akiteta jambo na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu wakati wa kuaga miili hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad