HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, April 1, 2017

MAHAKAMA KUU YAMWAMURU MSAJILI WA VYAMA VYA SIASA KUTOTOA RUZUKU KWA PROF. LIPUMBA NA KUNDI LAKE MPAKA SHAURI LITAKAPOAMULIWA

Mahakama Kuu imemuamuru Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kutotoa ruzuku kwa Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi, CUF, na kundi lake.

Zuio hilo ni mpaka shauri dhidi ya Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu kutoa fedha za ruzuku shilingi milioni 369 kwa njia za wizi na udanganyifu litakaposikilizwa na kutolewa maamuzi.

Uamuzi huo umefikiwa na Jaji Dyansobela baada ya kukubaliana na hoja zilizowasilishwa kwa hati ya dharura.

Jopo la Mawakili wa CUF, liliiomba Mahakama Kuu kutoa amri hiyo kwa kuwa fedha zilizotolewa awali shilingi milioni 369 hazijulikani zimetumika vipi, na hazikuwa katika mikono salama wala hakuna udhibiti wowote wa chama kuhusu fedha hizo ikizingatiwa kwamba, Prof. Lipumba alishavuliwa uanachama.

Mawakili hao akiwemo Juma Nassor , wamesisitiza kwamba, mazingira yaliyopo ni vyema na busara kwa fedha za umma zilizopaswa kutolewa kama ruzuku kwa chama cha CUF kwa sasa ziendelee kubakia serikalini.

Aidha, wameiomba Mahakama Kuu kwamba amri hiyo pia ifungamane na kesi ya msingi namba 23/2016 ya kuhoji maamuzi ya msajili kumtambua Prof Lipumba kwa nafasi ya uenyekiti iliyopo mbele ya Jaji Kihijo ambayo kwa sasa imekatiwa rufani ya kufanyiwa marejeo mbele ya Mahakama ya Rufani Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad