HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Monday, 3 April 2017

CHADEMA yavunja uongozi Wilaya ya Mtwara, mmoja atimkia CCM

Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kusini kikivunja uongozi wa Wilaya ya Mtwara na kuweka viongozi wa muda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Rwebangira Karuwasha ametangaza kuhamia CCM.
Mwenyekiti wa chama hicho wa Kanda ya Kusini ambaye pia ni Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe alisema jana kuwa, uamuzi huo umefikiwa baada ya kumalizika kwa kikao cha ushauri na wanachama kilichofanyika mjini humo.
Mwambe alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona kuna mgogoro uliosababisha kutokuwapo maelewano tangu wakati wa Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2015.
“Hatuwezi kuacha watu wagombane kwa miaka miwili hadi mitatu katika eneo lao, ni lazima hatua zichukuliwe. Tumeliona hili, tumeamua kuvunja uongozi uliopita na kuweka wa muda kwa ajili ya kukijenga chama na kuangalia namna tutakavyoweza kusonga mbele,” alisema Mwambe.
Mwenyekiti huyo alisema kamati ya ushauri inaendelea na kazi kuhakikisha majina ya watu wanne yanapatikana ambao mmoja kati yao atakuwa mwenyekiti na mwingine katibu. “Watu hawa watakuwa kwenye kikosi maalumu cha mpito kwa sababu Uchaguzi Mkuu wa kikatiba wa chama utafanyika mwezi Machi mwakani na hivi karibuni tumetoka katika mikutano ya Kamati Kuu tumekubaliana uchaguzi utafanyika mwezi huo,” alisema.
Mwanachama wa Chadema katika Manispaa ya Mtwara Mikindani ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalumu, Lulu Abdallah alisema wamefurahishwa na uamuzi huo kwa kuwa walikuwa na shida ya uongozi.
Mwenyekiti wa chama hicho katika Halmashauri ya Mtwara, Ismail Liuye alisema uongozi huo ulikaimishwa, hivyo ni sahihi kuvunjwa. Katika hatua nyingine, akizungumzia kuhamia CCM ikiwa ni siku chache baada ya Kamati Kuu ya Chadema kukutana mjini Tanga na kuvunja uongozi wa Wilaya ya Muheza, Karuwasha amesema ameamua kuhamia CCM ili kuendelea na siasa.
Akizungumza jijini Tanga jana, alisema ameamua kukihama chama hicho kwa kuwa uamuzi wa kuvunjwa kwa uongozi wao haukufuata utaratibu.
Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Tanga, Mathew Mganga alisema wamepokea taarifa kuhusu Karuwasha kuhamia katika chama chao na kwamba, wanamkaribisha kwa dhati.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad