HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 8, 2017

WANAWAKE JIKITENI KATIKA UJASIRIAMALI, UTAWAKOMBOA

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO.

Dunia ya sasa inapigania haki sawa kwa wanaume na wanawake ili waweze kushiriki kwa pamoja kwenye nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa ajili ya kuchangia kwenye ukuzaji wa pato la taifa na kupelekea kukua haraka kwa maendeleo ya nchi.

Tumeshuhudia wanawake wengi nchini wakijikita katika kufanya biashara na ujasiriamali wa bidhaa na huduma mbalimbali ambazo zinawakomboa kiuchumi na kuwafanya waweze kujitegemea kama walivyo wananume. 

Wanawake hao waliojiamini na kuamua kuanzisha biashara zao wameonekana kuwa na mafanikio makubwa ambayo yanasaidia kuinua uchumi wa mtu binafsi na wa nchi kwa ujumla.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wanawake wamekua bado hawana ujasiri wa kuanza kufanya ujasiriamali kwa kuhofia kuwa hawataweza kuendelea na wengine wakihofia waume zao kuwakataza.

Dhima ya kujirudisha nyuma waliyonayo baadhi ya wanawake ndio inayorudisha nyuma hata maendeleo ya nchi hasa kwa wakati huu ambao Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujikita katika kukuza uchumi wa viwanda.

Serikali inafanya jitihada mbalimbali za kuwahamasisha wanawake kufanya ujasiriamali hivyo kupitia Benki ya Wanawake, Serikali imeendelea kutoa huduma za mikopo kwa wajasiriamali wanawake nchini ili kuhakikisha wanapata mitaji ya kuanzishia shughuli hizo ambazo baadae zinakua ni mkombozi wa maisha yao.

Katika kipindi cha 2009 hadi 2014, Benki ya Wanawake imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya Shilingi bilioni 24.9 kwa wananchi 12,992 wakiwemo wanawake 11,350 ambayo ni sawa na asilimia 87.

Aidha, katika kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuinua hali zao kimaisha, Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake umenufaisha vikundi 3,119 vyenye jumla ya wanawake 23,769.

Idadi ya wanawake waliopata mikopo kutoka katika Mfuko huo  imeongezeka kutoka wanawake 3,008 mwaka 2005 hadi kufikia wanawake 23,769 mwaka 2014.

Pia jumla ya Mikoa 25 ya Tanzania Bara ilipelekewa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa ajili ya kuwakopesha wanawake, mikopo hiyo imewawezesha wajasiriamali wanawake kujiajiri katika shughuli mbalimbali za uzalishaji na hivyo kuinua kipato chao.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema kuwa jamii inatakiwa kuondokana na dhana ya mfumo dume inayomfanya mwanamke kukaa bila kufanya shughuli yoyote ya kiuchumi hivyo kuwa mtegemezi kwa kila kitu hali inayopelekea kushindwa kutoa maamuzi wanayoyataka na wengine kunyanyaswa.

Hivyo, jamii inatakiwa kuhakikisha inashirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuwajengea uwezo wanawake, kuwapa elimu na kuwapa fursa wanawake kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali zikiwemo za kilimo na biashara mbalimbali.

Ukiondoa mchango wa Serikali katika kuwasaidia wanawake kujikwamua, wanawake wenyewe kwa wenyewe wanatakiwa kusaidiana hasa wale walioendelea wanatakiwa kutoa elimu na ushauri kwa wanawake wenzao ili kila mwanamke afahamu juu ya umuhimu wa ujasiriamali na jinsi utakavyoweza kumkomboa katika maisha yake ya kila siku.

Pia wanashauriwa kujiunga katika vikundi vya kusaidiana ili kupeana mawazo mbalimbali ya biashara, kutiana moyo kwa kuwa siku zote mwanzo wa kitu chochote huwa ni mgumu pamoja na kusaidiana katika kupeana mitaji itakayowawezesha wajasiriamali kuinuka.

Kufuatia maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani,wanawake wa Tanzania wamepewa jukumu la kuhakikisha wanajikita katika ujasiriamali na kushiriki katika kuinua uchumi kupitia viwanda kwani wanawake ndio msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad