HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, March 7, 2017

WANAFUNZI SHULE YA SEKONDARI BARIADI WAANDAMANA KUPINGA KUHAMISHWA KWA MWALIMU WAO MKUU


Zaidi ya Wanafunzi 600 wa shule ya sekondari ya Bariadi Mkoani Simiyu wameandamana na kufunga barabara kuu ya Bariadi –Lamadi kupinga kuhamishwa kwa mkuu wa shule hiyo Deus Toga ambaye alipata uhamisho wa kwenda shule ya sekondari Giriku. 

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa tano asubuhi katika barabara hiyo na kusababisha kusimama kwa shughuli za mji huo ambapo lilidumu kwa muda wa masaa mawili hadi polisi walipoingilia kuwatawanya. 


Wanafunzi hao walikuwa wakiandamana kutoka shuleni kwenda katika ofisi ya mkurugenzi wa mji wa bariadi, umbali wa kilomita 1, lakini ilishindikana baada ya kikosi cha jeshi la polisi cha kuzuia ghasia (FFU) kuwadhibiti wanafunzi hao.

Aidha wanafunzi hao wakiwa katikati ya barabara waliamua kugeuka na kuandamana tena kuelekea ofisi ya mkuu wa mkoa  jambo lililoshindikana baada ya askari hao kuwazuia wakiwa wamefika eneo la Hospitali teule ya mkoa (somanda). 

Baada ya hali hiyo wanafunzi hao ambao ni wa kidato cha kwanza hadi cha sita waliamua kukaa katikati ya barabara huku wakimba nyimbo za kushinikiza kuwa hawamtaki mwalimu Paul Lutema ambaye alikuwa amepelekwa kuwa mwalimu mkuu wa shule hiyo badala ya mwalimu Toga. 


Wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe mbalimbali za kumkataa mwalimu Lutema na kumtaka mwalimu Toga wanafunzi hao walianza kuwarushia mawe askari hao wakitaka wasiwazuie kwenda katika ofisi ya mkuu wa mkoa hadi jeshi hilo walipoanza kuwarushia mabomu ya machozi.

Baada ya hali hiyo jeshi la polisi walipoanza kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi hao na kuwafukuza kurejea katika eneo la shule ambapo baadhi yao walikamatwa na kupigwa na kuwekwa ndani ya magari ya polisi wakipelekwa kituoni. 

Wakiongea na waandishi wa habari wanafunzi hao walisema kuwa walingiwa na mshituko asubuhi ya leo(jana) baada ya kutangaziwa kuwa mwalimu mkuu wao Deus Toga amehamishwa na wameletewa mwalimu Lutema. 

Walisema kuwa baada ya kutangaziwa hivyo waligoma kuingia madarasani na kuamua kuandamana kwenda ofisi ya mkurugenzi na ofisi ya mkuu wa mkoa wakitaka mwalimu mkuu huyo asihamishwe kutokana na uchapakazi wake toka amefika katika shule hiyo na ushirikiano aliounyesha shuleni hapo. 

“tangu mwalimu huyu kafika shuleni hapa ufaulu umeongezeka na migogoro ya shule iliyokuwepo haipo tena, na duka la shule lilikuwa limefungwa kutokana na migogoro ya walimu lakini toka amekuja hiyo migogoro imekwisha, ameunganisha walimu pia duka linafanya kazi’’Alisema Justine Mshana. 

Baadhi ya walimu wa shule hiyo ambao hawakutaka kutaja majina yao walisema kuwa wanafunzi hao ni vema wakasikilizwa kwani madai yao ni ya msingi hawawezi kugoma tu bila sababu ya msingi. 

Baada ya tukio hilo kaimu mkuu wa mkoa wa Simiyu ambaye ni mkuu wa wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga na Afisa elimu wa Mkoa Julius Nestory walifika shuleni hapo kuwatuliza wanafunzi hao kwa kuwataka warudi darasani huku suala lao likishughulikiwa haraka. 

Kiswaga aliwataka wanafunzi warejee madarasani wakaendee na masomo kwani madai yao yamekubaliwa na kwamba mwalimu huyo hatamishwa na atabaki katika shule hiyo.

Kwa upande wake afisa elimu huyo alisema kuwa ofisi ya mkurugenzi ilifanya mamuzi yasiyo sahihi bila kuzingatia sheria na taratibu za uhamisho kwa sababu mwenyemamlaka wa kuwahamisha wakuu wa shule ni katibu tawala wa mkoa. 


“ofisi ya katibu tawala na ofisi yangu hatujapata na taarifa ya uhamisho huu hivyo tumeamua kutengua maamuzi ya ofisi ya mkurugenzi na tunawataka viongozi wenzangu wasifanye maamuzi bila kufuata utaratibu na sheria”alisema Nestory.  Habari na Shushu Joel.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad