HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 13, 2017

WADAU WA BARABARA WATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUDHIBITI AJALI NCHINI

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akizungumza na wadau waliohudhuria mkutano wa siku mbili wa Usalama barabarani katika ukumbi wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es salaam.
 Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini (RFB) Bw. Joseph Haule akitoa taarifa ya udhibiti wa ajali za barabarani kwenye mkutano wa wadau wa usalama barabarani uliofanyika jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akiongea na Naibu Waziri wa Ujenzi na Mawasiliano wa Namibia Mhe. Sankwasa James Sankwasa wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akizungumza na Mwenyekiti wa Chama cha Kimataifa kinachoshughulika na masuala ya barabara  Dkt. Kiran Kapila wakati wa mkutano wa siku mbili wa kutathmini usalama barabarani, Jijini Dar es salaam.
 Mmoja wa wanafunzi aliyeshinda tuzo ya uchoraji wa picha ya usalama barabarani Veronica Shirima akitoa maelezo kwa wadau wa usalama barabarani, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wanne kulia) akiwa katika picha ya pamoja na wadau wa Usalama barabarani mara baada ya kufungua mkutano huo, Jijini Dar es salaam.
Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wadau wa usafirishaji kuweka mikakati dhabiti ya kupunguza ajali za barabarani nchini ili kuokoa maisha ya watanzania wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na ajali hizo.
Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo alipofungua mkutano maalumu wa kanda wa kujadili na kutathmini changamoto za usalama barabarani na jinsi ya kuzikabili unaofanyika jijini Dar es salaam.
Profesa Mbarawa amesema kuwa ajali za barabarani zimekuwa zikikatisha maisha ya watanzania wengi kila mwaka ambao wengi wao ni vijana na nguvu kazi ya taifa hivyo ni jukumu la wadau kubadilisha hali ya usalama barabarani.
“Kama tukijifunza vizuri na kuyafanyia kazi mafunzo haya tunaweza kubadili hali ya usalama barabarani kwani inaumiza kuona vifo vya watu wengi vinavyotokana na ajali za barabarani hivyo ni wakati wa Jeshi la Polisi, na  Mamlaka ya Usafiri wa nchi Kavu na Majini SUMATRA kushirikiana kukomesha ajali hizi”. Amesisitiza Profesa Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali itatoa kipaumbele kwa yale yatakayojadiliwa na kuamuliwa katika mkutano huo ili kuongeza kasi ya udhibiti wa ajali za barabarani hapa nchini na kupunguza idadi ya ajali zinazoepukika.
Naye Mwenyekiti wa Mfuko wa Barabara nchini (RFB), Bw. Joseph Haule amesema kuwa Bodi hiyo inashirikiana na taasisi nyingine katika kuhakikisha ubora wa miundombinu ya barabara inakuwa salama na kupitika wakati wote.
Kwa upande wake Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani hapa nchini Mohamed Mpinga amesema kikosi cha usalama barabarani kitaendelea kuhakikisha kuwa ajali za barabara zinadhibitiwa.
“Suala la ajali za barabarani ni jukumu letu sote kwa pamoja hivyo tukiungana kwa pamoja na kushirikiana tutaweza kupunguza ajali hizi kwa kiwango kikubwa”.  Amesema Kamanda Mpinga.
Mkutano huo wa siku mbili ulioanza leo jijini Dar es salaam umewakutanisha wadaau mbalimbali wa kimataifa wa masuala ya ujenzi na usimamizi wa usalama wa watu na mali wawapo barabarani .
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad