HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 27, 2017

WAZIRI MKUU MAJALIWA APOKEA TAARIFA YA TUME YA FARU JOHN

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea  kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele  taarifa ya Tume aliyoiunda ya kuchunguza suala la Faru John, ofisini kwake jijjini Dar es salaam Machi 27, 2017. (Picha na Ofisi ya `Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkemia Mkuu wa Serikali , Profesa Samwel Manyele wakati  alipowasilisha taarifa ya tume ya uchunguzi wa suala Faru John baada ya kukabidhi taarifa hiyo , Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Machi27, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kukabidhiwa taarifa ya tume ya kuchunguza suala la Faru John na Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Samwel Manyele, Ofisini kwake jijini Dar es salam Machi 27, 2017.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu amepokea taarifa hiyo, leo (Jumatatu, Machi 27, 2017) kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni dume.

Prof. Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.

“Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake,” amesema.

Prof. Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.  

Mengine ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.

Pamoja na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema Prof. Manyele katika ripoti yake.  

Akizungumzia kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi, Prof. Manyele amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri  na kwamba tume inashauri TAWIRI na TANAPA wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.

Amesema kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na tafiti ili kulinda taarifa muhimu za vinasaba vya wanyamapori (Genetic information) dhidi ya mataifa mengine. “TUME inashauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe kitengo cha Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA Forensic Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake iweze kufanya maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa kimahakama katika kesi za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru timu ya uchunguzi iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu uliokuwemo ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.

“Ofisi yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha Serikali imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa.”

Alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.

Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea pembe mbili za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha faru huyo. Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika kumhamisha faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.

Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi mkoani humo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, MACHI 27, 2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad