HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, March 1, 2017

JESHI LA POLISI MKOANI ARUSHA LAWATAKA WANAFUNZI KUWA MAKINI

Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha

Wanafunzi wa shule za Msingi mkoani hapa wametakiwa kuwa makini na kutokuwa na tamaa ya kuomba “lift” au kupewa chipsi au kushawishiwa kwa namna yoyote ile na watu ambao hawafahamiana nao pindi wanapokwenda shule au wanaporudi majumbani kwao.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu wakati alipokuwa akitoa elimu ya Ukatili na Unyanyasaji wa kijinsia katika vipengele vya ubakaji, ulawiti na vipigo kwa wanafunzi 63 wa Elimu Maalum kitengo cha viziwi katika shule ya Msingi Meru iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.

Alisema baadhi ya wanafunzi wanajikuta wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kama ubakaji na ulawiti baada ya ushawishi mdogo mdogo kwa kupewa lift, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi na kadhalika. 
Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu akiwa katika picha ya pamoja na Walimu na Wanafunzi wa shule ya Msingi Meru kitengo cha elimu maalum.

“Baadhi ya vitu ambavyo vinasababisha ushawishi na hatimaye wanafunzi wanafanyiwa ukatili wa kubakwa au kulawitiwa bila hata wao wenyewe kudhani kama hali hiyo inaweza kutokea ni pamoja na lift za magari au pikipiki, kununuliwa vyakula mbalimbali kama vile chipsi.”. Alisema Mkuu huyo wa Dawati Happyness Temu.

“Sio watu wote wana nia mbaya katika utoaji wa “lift” ila kuna wachache si wema na hawawezi kujulikana  yupi mwema na yupi mbaya hivyo wazazi wanatakiwa wawafuatilie kwa ukaribu na kuwaeleza uhalisia wa mabadiliko ya maisha watoto wao ili kuwaepusha na watu wenye nia mbaya dhidi yao”. Aliongeza Mkaguzi huyo wa Polisi Happyness Temu.

Wakiongea kwa lugha ya ishara na kutafsiriwa na walimu wa shule hiyo Veila Wilson na John Maukiri, baadhi ya wanafunzi walionyesha kufurahia elimu hiyo na kupata ufahamu juu ya hatua wanazoweza kuchukua katika kujiepusha na vitendo vya ukatili na unyanyasaji na pia walifahamu hatua za kuchukua mara watakapofanyiwa ukatili wa aina yoyote.
Mwalimu Veira Wilson katikati akiwa anaongea kwa ishara wakati anawatafsiria wanafunzi wa elimu maalum (Viziwi) uelimishaji uliokuwa unatolewa na Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu ambaye yupo kulia kwake na kushoto kwake ni Mwalimu John Maukiri .

Baadhi ya wanafunzi hao walikiri kufanyiwa hasa ukatili wa vipigo majumbani mwao huku mkuu huyo wa Dawati kuahidi kuwasilikiza walalamikaji na kufuatilia kwa ukaribu kwa nia ya kukomesha tabia hiyo.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambayo inamchanganyiko wa wanafunzi wa elimu ya kawaida na elimu maalum Bw.Musa Luambano, alilishukuru Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto kwa kutoa elimu hiyo kwa wanafunzi hao ambayo itawasaidia kujua hatua za kuchukua pindi wanapofanyiwa ukatili lakini pia wao watakuwa mabalozi kwa wengine katika kuwaelimisha.

Alisema kitendo cha Jeshi la Polisi kufika katika shule hiyo na kutoa elimu kwa wanafunzi wa kitengo cha elimu maalum ni ishara ya hatua nzuri katika kuongeza ushirikiano kati ya Jeshi hilo na wanafunzi wa aina hiyo na kutoa wito kwa ofisi mbalimbali kupeleka watumishi wao ili waweze kujifunza elimu ya lugha ishara ambayo itaweza kuwasaidia katika kuhudumia makundi yenye uhitaji maalum kama vile viziwi.
Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu akitoa somo juu ya ukatili na unyanyasaji wa jinsia kwa wanafunzi wa elimu maalum katika shule ya Msingi Meru iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.
Mkuu wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto mkoa wa Arusha Mkaguzi wa Polisi Happyness Temu akiagana na wanafunzi wa shule ya Msingi Meru kitengo maalum mara baada ya kuwaelimisha juu ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad