HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 15 February 2017

WAZIRI MKUU AWAAGIZA DC, DED KITETO WAKAJIBU KERO ZA WANANCHI JUMAMOSI

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto mjini Kibaya akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya mkoa wa Manyara, Februari 15, 2017.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Eng. Tumaini Magesa na Mkurugenzi wa Halmsahuri ya wilaya hiyo, Bw. Tamim Kambona waende kata ya Engusero Jumamosi wiki hii wakafanye mkutano wa hadhara na kujibu kero za wananchi wa kata hiyo.

Mkuu wa Wilaya hiyo na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo wametakiwa pia wafuatane na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Bw. Lairumbe Mollel wakatoe ufafanuzi bila kukosa.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Februari 15, 2017) katika kijiji cha Engusero wilayani kiteto baada ya kusimamishwa na wananchi wakati akiwa njiani kuelekea mjini Kibaya yalipo makao makuu ya wilaya hiyo ili aanze ziara ya kikazi ya mkoa wa Manyara.

Akijibu baadhi ya maswali aliyoulizwa na wananchi wa kijiji cha Engusero, Waziri Mkuu amesema analichukua ombi la wakazi hao la kupata kujengewa soko la kimataifa katika kata hiyo ili waweze kuuza mahindi hapo hapo.

“Nitaawagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri waje hapa Jumamosi hii na kufanya mkutano ili wawaeleze wana mpango gani kuhusiana na ujenzi wa soko hilo,” amesema.

Awali , Mkazi wa kata hiyo Bw. Ali Athumani alimuomba Waziri Mkuu awasiaidie ili wajengewe soko la kimataifa kwa sababu wao ni wazlishaji wakubwa wa mahindi lakini hawafaidiki nayo kwa sababu yote yanaenda kuuzwa katika soko la Kibaigwa.

Naye Bw. Said Shabani alimuomba Waziri Mkuu awasaidie kufuatilia upatikanaji wa gari la wagonjwa na ujenzi wa wodi nyingine ya wagonjwa pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti kwenye zahanati yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka nia ya dhati ya kupambana na dawa za kulevya na amewataka watendaji wote kuanzia ngazi ya vijiji wadhibiti suala hilo.

“Serikali haiwezi kuona vijana wanaangamia kwa dawa za kulevya. Tumeamua kudhibiti hali hiyo. Hii vita ni ya nchi nzima. Kuanzia sasa, viongozi wa Serikali za vijiji wakamateni wale wote wanaojihusisha na biashara hii.”

“Tunataka vijiji vyetu, kata zetu, wilaya zetu na mikoa yetu iwe safi bila hata chembe ya dawa za kulevya. Tukikuona kijana unayumbayumba au kuweweseka, tunakupima na tukikuta umetumia ile kitu, tunakukamata ili utuambie ni nani amekupa,” amesema na kuongea:

“Sisi tunataka vijana wafanye kazi za kujiletea maendeleo. Kijana hawezi kuwa na maendeleo wakati hufanyi kazi, huwezi kuwa na ndoto za maendeleo wakati umelewa bangi au dawa za kulevya. Kila mmoja afanye kazi kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu,” amesisitiza.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Engusero wilayani Kiteto waliofunga barabara wakitaka asimame kuwasalimia. Alikuwa kitoka Dodoma kwenda Kiteto kwa ziara ya kazi mkoani Manyara Februari 15, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akivalishwa skafu baada ya kuwasili mjini Kibaya kuanza ziara ya kazi wilayani Kiteto Februari 15, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Katibu Tawala wa mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi baada ya kuwasili mjini Kibaya kuanza ziara ya wilaya ya Kiteto Februari 15, 2017.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimina na viongozi wa dini baada ya kuwasili mjini Kibaya kuanza ziara ya wilaya ya Kiteto Februari 15, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bendera tarifa ya mkoa wa Manyara baad ya kusomewa mjini Kibaya katika siku ya kwanza ya ziara yake wilayani Kiteto Februari 15, 2017.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto mjini Kibaya akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake wilayani Kiteto Februari 15, 2017. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joel Bndera na kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Eliakim Maswi.

.
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao mjini Kibaya Februari 15, 2017. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad