HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 16, 2017

UMOJA WA ULAYA WASAIDIA MRADI WA LISHE NA USALAMA WA CHAKULA WA WFP KATIKA MIKOA YA KANDA YA KATI, TANZANIA

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula  Dunini (WFP) limepokea mchango wa Euro (€) milioni 9.5 kutoka Umoja wa Ulaya (EU) kwa lengo la kuunga mkono Mradi wenye thamani ya Euro milioni 24.5 (takribani Shilingi za Tanzania bilioni 50) wa kusaidia kukuza Usalama wa Chakula na Lishe katika mikoa ya kati nchini Tanzania.

Mradi umeandaliwa ili kuimarisha usalama wa chakula na lishe kwa watu wapatao 40,000  na wakati huohuo ukichangia katika kupunguza utapiamlo katika wilaya zinazolengwa za Bahi na Chamwino mkoani Dodoma na Ikungi na Singida Vijijini katika mkoa wa Singida. 

Mchango wa EU umetangazwa leo wakati wa hafla ya kutiliana saini makubaliano katika Jengo la Umoja jijini Dar es Salaam uliofanywa na Dr. Mpoki Ulisubisya, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Michael Dunford, Mwakilishi wa WFP nchini Tanzania na Roeland Van De Geer, Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania.

“Licha ya kuimarika kwa viashiria vingi vya afya katika muongo uliopita, bado hakuna hatua kubwa katika kuimarisha hali ya lishe ya watoto na wanawake nchini Tanzania,” Roeland Van De Geer, Mkuu wa Ubalozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, alisema wakati wa hafla hiyo".

“Viwango vya juu vya kudumaa, kukosa uzito wa kuridhisha na upungufu wa viinilishe nchini kunaashiria dharura ya kimyakimya. Utayari wa kisiasa katika safu ya viongozi wa juu katika kukabili lishe duni nchini Tanzania kwa mtazamo wa sekta nyingi kwa hakika ni mageuzi makubwa. Kupitia mradi huu, EU pamoja na WFP ziko katika nafasi nzuri ya kubaini na kuunga mkono uhusiano kati ya kilimo, afya, usalama wa chakula na lishe, ambao hapo kabla haukuwa umeelezwa kwa kina au kufuatiliwa kikamilifu.”

Mradi huu unatumia uwepo wa muda mrefu wa WFP katika mikoa ya kati nchini Tanzania na uzoefu wake katika kutoa chakula chenye lishe na mawasiliano yenye lengo la kubadilisha tabia ya kijamii kupitia vituo vya afya. Shughuli hizi zitakamilishwa na jitihada katika sekta nyingine ili kutoa mtazamo ulio kamili zaidi wa kupunguza kudumaa nchini. Viwango vya Taifa vya kudumaa viko katika asilimia 34 ambapo kwa Dodoma ni asilimia 36.5 na Singida ni asilimia 29.2

“Tunashukuru kwa mchango huu kutoka Umoja wa Ulaya kwani umeiwezesha WFP kuendelea na programu hii bunifu inayolenga kukidhi mahitaji ya watu walio hatarini zaidi, hasa watoto katika kile kipindi muhimu sana cha ukuaji wao, yaani siku 1,000 za mwanzo tangu kubebwa mimba hadi kutimiza miaka miwili,” Mwakilishi wa WFP Michael Dunford alisema katika hafla hiyo. “Programu hii itatoa ushahidi ambao utatoa mwongozo kwa jitihada za baadaye, na kwa hiyo ina uwezekano wa kuleta mabadiliko ya kudumu nchini Tanzania.”

Nchini Tanzania, viwango vya utapiamlo sugu miongoni mwa watoto unatokana na umaskini, ukosefu wa usalama wa chakula na ukosefu wa chakula cha kutosha kwa watoto wachanga na unyonyeshaji watoto. Mradi utalenga kukuza maarifa kuhusu lishe, mtawanyiko wa lishe na taratibu za kutumia maji, usafi wa mazingira na usafi wa mwili (WASH). Shughuli hizi zitapewa nguvu kwa kuhamasisha ufugaji wa idadi inayofaa ya mifugo, kupanda mazao tofautitofauti na kuhamasisha vijiji kuanzisha vikundi vya kuweka akiba na kukopa, yote yakilenga kukuza uwezekano wa kupata mtaji.

Shirika la Save the Children ni mshirika wa WFP katika kuimarisha ushirikiano na uwezo wa asasi zilizojikita katika jamii ili kuhamasisha uwezeshaji wa jinsia na uhusiano wa sekta mbalimbali katika suala la lishe, pamoja na kuratibu utekelezaji wa kipengele cha kilimo katika mradi.

Kwa kuratibu shughuli hizi chini ya mwamvuli wa WFP, Umoja wa Ulaya na Shirika la Save the Children zitakuwa zikishughulikia changamoto nyingi zinazolenga kuimarisha usalama wa chakula na lishe nchini Tanzania.

Mradi huu ni sehemu ya majukumu ya WFP katika kufanikisha Lengo la 2 katika Malengo ya Maendeleo Endelevu: Kufuta Njaa. Ili Kuondoa Njaa kabisa ifikapo mwaka 2030, WFP inashirikiana na washirika mbalimbali kama vile serikali, sekta binafsi na vyama vya kiraia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad