HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 10, 2017

TGGA KUADHIMISHA ‘THINKING DAY’ KWA KUFANYA SHUGHULI ZA KIJAMII

 Kamishna wa Makao Makuu wa Tanzania Girl Guides Association (TGGA), Rosaldina Majuva alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya chama hicho wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, kutoka kulia Kamishna Mkuu wa chama hicho Symphorosa Hangi na Katibu wa chama hicho, Grace Shaba.
Katibu wa chama cha Tanzania Girl Guides Association (TGGA), Grace Shaba akifafanua kuhusu malengo ya chama hicho wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, kulia ni  Kamishna Mkuu wa chama hicho Symphorosa Hangi, kushoto ni  Kamishna wa Makao Makuu wa chama hicho, Rosaldina Majuva.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
 Tanzania Girl Guides Association (TGGA) wanategemea kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa chama hicho kwa njia ya kufanya shughuli mbalimbali za kuisaidia jamii.

Maadhimisho hayo yanayojulikana kama ‘thinking day’ yatafanyika Februari 22 mwaka huu ambapo shughuli za kuisaidia jamii zitaanza Februari 10 mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Makao Makuu wa Chama hicho, Rosaldina Majuva alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho hayo.

Bi. Rosaldina amesema kuwa siku ya maadhimisho ya chama hicho inaambatana na siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa waasisi wao akiwemo Lord Baden Powell ambaye alikuwa kiongozi wa Boy Scout pamoja na Kamishna Mkuu wa Girl Guides na Girl Scouts, Lady Olave Baden Powell (mkewe).

“Tumepanga kuadhimisha siku hii muhimu kwa kufanya shughuli za kijamii zikiwemo za kutoa misaada kwa wahitaji, kutunza mazingira kwa kufanya usafi katika eneo la Coco Beach na Magomeni na kupanda miti, kutoa elimu ya kujithamini, kujitambua na kukataza unyanyasaji pamoja na kutembelea kituo cha wazee wa Kigamboni,”alisema Bi. Rosaldina.

Kwa upande wake Katibu wa chama hicho, Grace Shaba amefafanua kuwa chama hicho kimelenga kupanua uelewa wa wanawake kwa ujumla kuhusu uzalendo, majukumu ya nchi yao, kujenga ushirikiano wa kitaifa na kimataifa kupitia kambi za mafunzo, kutembelea na kuwasiliana kwa njia za teknohama pamoja na kuwa tayari kufanya kazi kwa manufaa yao na ya Taifa.

“Dira yetu ni kuwa na jamii yenye wasichana na wanawake waliowezeshwa kufikia uwezo wa juu kabisa katika kutimiza malengo yao na kuwa rasilimali bora ya Taifa,”alisema Bi. Grace.

Nae Kamishna Mkuu wa Tanzania Girl Guides Association, Symphorosa Hangi amesisitiza wanawake na watoto wa kike kujiunga na chama hicho kwani kinatoa elimu ya masuala ya kijamii na kiuchumi yatakayosaidia kuwainua wanawake na watoto pamoja na taifa kwa ujumla.

Mpaka sasa kwa Tanzania,chama hicho kipo katika mikoa 22 kikiwa na jumla ya wanachama 101,824.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad