HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 1 February 2017

SAKATA SHAMBA LA MBOWE SASA LAIBUA MENGINE

Hatua ya Serikali kumtaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kusitisha mradi wa kilimo cha kisasa kwa madai kuwa shamba lake liko kwenye chanzo cha maji imeibua hisia tofauti, ikihusishwa na nyingine zilizochukuliwa dhidi yake kwenye miradi mingine.
Kabla ya hatua hiyo, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alipewa siku 14 kulipa kodi katika hoteli yake iliyoko jimboni humo na kabla ya hapo alihamishwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwenye jengo la Bilicanas, ikielezwa kuwa anadaiwa kodi ya pango wakati mwenyewe akisema alikuwa mmiliki mwenza.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gellasius Byakanwa amempa Mbowe miezi minne kuondoa mazao yote yaliyopo katika shamba hilo linalodaiwa kuwa ndani ya mita 60 karibu na Mto Weruweru, vinginevyo achukuliwe hatua za kisheria.
Wakili wa kujitegemea, Frank Robert aliitaka Serikali kusimamia sheria pasipo upendeleo wala ubaguzi ili jamii isitafsiri kama hatua inazozichukua zinalenga kudhibiti upinzani.
Alitolea mfano nyumba zaidi ya 160 zikiwamo za vigogo wa taasisi za umma na wastaafu katika mji wa Moshi ambazo zinadaiwa kujengwa ndani ya mita 60 katika mito ya Karanga na Rau.
Alisema anakumbuka Desemba 2015, aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Novatus Makunga alitangaza mpango wa Serikali kubomoa nyumba hizo lakini hakuna iliyobomolewa.
Hata hivyo, Wakili mwingine, Peter Mshikilwa alisisitiza kuwa ni makosa shughuli za maendeleo na kijamii kufanyika katika maeneo ya vyanzo vya maji na kwamba huo ni msimamo wa sheria kwa wote na si watu fulani tu.
Mbunge wa Moshi Vijijini (Chadema), Anthony Komu alidai anachofanyiwa Mbowe ni uhasama wa kisiasa zaidi kuliko kusimamia sheria na kutolea mfano wa nyumba hizo 160 za mjini Moshi.
Mbowe alipoulizwa na gazeti hili kuhusu sakata hilo, aliomba asizungumze chochote.

Nyumba 160
Februari 17 mwaka jana, Ofisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Seperatus Rutagenya alithibitishia gazeti hili kuanza kwa mchakato wa kubomoa nyumba hizo 160.
“Zoezi la kwanza lilikuwa ni kutambua watu walioingia ndani ya mita 60 na tumebaini nyumba zaidi ya 100 Mto Karanga na zaidi ya 60 kule Mto Rau,” alisema.
Alisema mchakati huo umeingia hatua ya pili ambayo ni kuwabaini kwa majina wamiliki wa nyumba hizo na kazi hiyo inatarajiwa kuwa limekamilika kufikia Febrauri 19.
Alisema pamoja na sheria kuwa wazi na Serikali kutangaza bomoabomoa, bado wapo watu ambao wameanza ujenzi upya ndani ya mita 60 na kuhoji wanapata wapi ujasiri huo.

Sakata la Bilicanas, hoteli
Uamuzi wa NHC kumwondoa Mbowe katika Jengo la Bilicanas, jijini Dar es Salaam na kutishia kufunga hoteli yake iliyopo Hai yamehusishwa na vita ya kisiasa ikidaiwa kwamba utekelezaji wake umemlenga Mbowe huku wengine wakiachwa.
Septemba Mosi mwaka jana, NHC ilitoa vifaa vyote vinavyotumiwa na Kampuni ya Free Media na kufungua vifaa vyote vya muziki kwenye klabu maarufu ya Bilicanas kwa madai kuwa anadaiwa pango zaidi ya Sh1.17 bilioni.
NHC pia ilitangaza wadaiwa wengine sugu ikisema wangechukuliwa hatua kama hiyo lakini hadi sasa hazijachukuliwa.
Alipotafutwa kwa simu jana, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu alipokea na baada ya kuulizwa kuhusu suala hili alisema yuko kikaoni, hivyo asingeweza kuzungumza. Baadaye aliomba atumiwe ujumbe mfupi lakini baada ya kutumiwa hakujibu.
Awali, Mchechu alisema Mbowe alikuwa ni miongoni mwa waliopewa notisi na hatua hiyo haina uhusiano wowote na masuala ya kisiasa.
Mwenyekiti mstaafu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji mstaafu Amir Manento alisema asingependa kuzungumzia suala la Mbowe na NHC. Hata hivyo, alisema jambo la msingi haki lazima itolewe kwa wote.
“Naomba nizungumzie upande wa sheria inasemaje, kama sheria inawaruhusu NHC ni sahihi kumwondoa yeyote na katika masuala ya utekelezaji wa sheria huwezi kusema eti mbona fulani hajaondolewa. Pia, suala lao liliamuliwa na mahakama kwa hivyo kuna haki ilitendeka,” alisema Jaji Manento.
Mshauri wa masuala ya jinsia na mwanaharakati wa haki za binadamu, Gemma Akilimali alisema hatua zozote zinazochukuliwa na Serikali zinatakiwa kutekelezwa bila kuhusisha sura ya mtu. Alisema inapotokea kundi moja au upande fulani umeachwa inajenga wasiwasi kwenye jamii.
“Sisi tunaofuatilia tunapata wasiwasi kama zoezi lilikuwa ni genuine (halisi) au lilikuwa linalenga mtu mmoja tu, haitakiwi kuacha yeyote yule,” alisema.

CHANZO: MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad