HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 16 February 2017

PROFESA NTALIKWA AKUTANA NA UJUMBE WA WAZIRI MKUU WA UINGEREZA

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) na Mwakilishi wa  Waziri Mkuu wa Uingereza anayehusika na masuala ya Biashara nchini Kenya na Tanzania,  Lord Hollick  wakimsikiliza mmoja wa Wataalam wa Wizara ya Nishati na Madini (hayupo pichani) wakati wa kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (kulia) akimsikiliza Balozi wa Uingereza nchini Tanzania  Sarah Cooke, (kushoto)  aliyeambatana Mwakilishi wa  Waziri Mkuu wa Uingereza anayehusika na masuala ya Biashara nchini Kenya na Tanzania,  Lord Hollick (katikati). kikao kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Nishati na Madini jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa (katikati) akiongoza kikao baina ya Ujumbe kutoka nchini Uingereza ukiongozwa na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania  Sarah Cooke pamoja Watendaji mbalimbali wa Idara ya Nishati katika Wizara ya Nishati na Madini.

Na Teresia Mhagama, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa Justin Ntalikwa tarehe 16 Februari, 2017  amekutana na Ujumbe kutoka Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania ukiongozwa na Balozi,  Sarah Cooke,  aliyeambatana  na Mwakilishi wa  Waziri Mkuu wa Uingereza anayehusika na masuala ya Biashara nchini Kenya na Tanzania,  Lord Hollick na Mshauri wa Hali ya Hewa na Mazingira.
Katika kikao hicho walijadili masuala mbalimbali ikiwemo upunguzaji wa madeni ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ili Shirika hilo liweze kujiendesha lenyewe kwa ufanisi pamoja uendelezaji wa miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Profesa Ntalikwa pia aliueleza Ujumbe huo kuhusu mipango inayofanywa na Serikali ya kuendeleza miradi mbalimbali ya umeme ikiwemo uandaaji wa kabrasha litakaloainisha  miradi yote ya umeme inayohitaji wawekezaji.
Alisema kuwa kabrasha hilo litasambazwa kwa wadau mbalimbali na wawekezaji ili waweze kulisoma na kufanya maamuzi ya kuwekeza kwenye miradi husika.
“Kabrasha hilo limeshaandaliwa na Wataalam na kwa sasa linapitiwa na baadhi ya Taasisi za Serikali  kabla ya kulisambaza kwa wadau wetu kupitia njia mbalimbali kama Tovuti na magazeti,” alisema Profesa Ntalikwa.
Kwa upande wake,  Mwakilishi wa  Waziri Mkuu wa Uingereza anayehusika na masuala ya Biashara nchini Tanzania,  Lord Hollick alisema kuwa kipaumbele cha nchi hiyo ni kuwekeza kwenye miradi ya nishati kwani Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati jadidifu  ikiwamo, Jotoardhi, maporomoko madogo ya Maji, Tungamotaka, Jua na Upepo.
“ Tunao mtaji wa kuwekeza kwenye miradi ya umeme na pia tunaweza kusaidia kiutaalam ili kuifanya TANESCO kufanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza changamoto mbalimbali zinazochelesha uwekezaji,” alisema  Hollick.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad