Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), akipata taarifa ya maendeleo ya Uwanja wa Ndege wa Mtwara kutoka kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoani humo, Bi. Zitta Majinge (kulia), mara baada ya kuwasili leo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa tatu kulia), akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoa wa Mtwara, Bi. Zitta Majinge (wa pili kulia), kuhusu ukarabati wa uwanja huo mara baada ya kuwasili leo mkoani hapo. Kushoto kwa Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Bw. Evod Mmanda.
Muonekano wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara ambalo lina uwezo wa kubeba abiria 100 kwa wakati mmoja.
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoa wa Mtwara, Bi. Zitta Majinge (katikati), akimuonesha Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kulia), mipaka ya Uwanja wa Ndege huo ambao unahitajika kuwekwa uzio ili kulinda usalama wa uwanja.
Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara yenye urefu wa mita 2258 na upana wa mita 30.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (kushoto), akifafanua jambo kwa Meneja wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) mkoa wa Mtwara Emmanuel Wanje, wakati alipokagua Uwanja wa Ndege wa Mtwara leo.
Serikali
imesema ina mpango wa kukarabati uwanja wa ndege wa Mtwara
ifikapo mwezi Julai mwaka huu ili kuruhusu ndege kubwa kuweza kutua uwanjani
hapo na hivyo kufungua fursa za kiuchumi mkoani humo.
Akizungumza
mara baada ya kukagua uwanja huo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Profesa Makame Mbarawa, amesema kuwa ukarabati huo utahusisha njia ya kuruka na
kutua ndege, maeneo ya maegesho pamoja na barabara yenye urefu wa km 1.5
inayoingia katika uwanja huo.
"Tunategemea
mwisho wa mwezi huu kutangaza zabuni ya ukarabati wa uwanja huu, matumaini yetu
tutampata mkandarasi mzuri kwa ajili ya kazi hii", amesema Waziri Mbarawa.
Aidha,
Profesa Mbarawa amefafanua kuwa Serikali itahakikisha kuwa inajenga uzio katika uwanja huo ili kuhakikisha
usalama wa uhakika uwanjani hapo.
Sambamba na hilo, Waziri Mbarawa
ametanabaisha kuwa Serikali ina mpango wa ununuzi wa rada nne mpya kubwa
na za kisasa ili kubaini taarifa za ndege nchini tangu zinapoanza kuruka hadi kutua.
“Tukiwa na rada kubwa na za kisasa
zitatusaidia kubaini ndege zote hata ndogo zinazoingia katika maeneo ya viwanja
vya madini kwa lengo la kuona ndege hizi zinaingia na zinatoka na nini?”,
amesisitiza Waziri Mbarawa.
Kuhusu
ujio wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Bombadier Q 400, Waziri huyo amemhakikishia Mkuu wa Wilaya ya
Mtwara, Evod Mmanda, kuwa Serikali
inatarajia kuanzisha safari zake kutoka Dar- Mtwara na Songea hivi karibuni.
Kwa
upande wake Mkuu wa wilaya hiyo, amemuomba Waziri huyo kuharakisha ujio wa
ndege hizo ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa Mtwara na kuchochea fursa za
kibiashara katika Mkoa huo na mikoa ya jirani.
Naye
Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania(TAA) mkoa wa Mtwara, Bi.
Zitta Majinge, amesema kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na Serikali
kuhakikisha kuwa uboreshaji wa miundombinu ya viwanja hivyo inafanyika kwa
wakati ili kukidhi mahitaji ya wasafiri wa anga.
Katika
hatua nyingine, Profesa Mbarawa amekagua maendeleo ya Kivuko cha MV Kilambo
kinachotoa huduma kati ya Kilambo na Namoto nchini Msumbiji na kuhakikisha kuwa
kivuko hicho kinafanya kazi katika vipindi vyote vya mwaka.
Waziri
Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Mtwara ambapo
ametembelea na kukagua miradi mbalimbali inayosimamiwa na Wizara yake.
Imetolewa na
Kitengo cha Mawasiliano, Serikalini Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment