HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 17 February 2017

NAPENDA SOKA LA KUSHAMBULIA, SIO LA KUJILINDA- KOCHA AZAM

 Kocha Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Aristica Cioaba

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

BAADA ya kupata kibali cha kufanya kazi nchini juzi, Kocha Mkuu wa Klabu ya Azam FC, Aristica Cioaba, amejinasibu ya kuwa yeye ni aina ya kocha anayependa falsafa ya soka la kushambulia na sio kujilinda.

Cioaba aliyesaini mkataba wa kuinoa Azam FC mwezi mmoja na nusu uliopita, ameweka wazi hayo mara baada ya mchezo wao wa kirafiki na timu ya  Red Arrows ya Zambia na kuondoka na ushindi wa goli 1-0 ikiwa ni mechi yake ya kwanza kuiongoza kama Kocha Mkuu wa benchi la Ufundi.

“Mimi ni kocha ninayependa soka la kushambulia, sio aina ya kocha ninayependa timu yangu icheze kwenye eneo la kujilinda, napenda kuwapa mabao mengi mashabiki wanaokuja uwanjani kushuhudia mechi na kuwafanya baada ya mechi wawe na furaha.

Kocha huyo wa zamani wa Aduana Stars ya Ghana, alisema kuwa mchezo huo ulikuwa mzuri sana na anafuraha kubwa baada ya wachezaji wake kucheza vizuri na kwa nguvu muda wote pamoja na kupata matokeo mazuri ya ushindi.

“Ninapenda sana mechi nyingi za kimataifa za kirafiki kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho), hii ni mipango yetu ya baadaye na kila mtu ananielewa mimi, nimekuja hapa mwezi mmoja na nusu uliopita, kibali change cha kazi kimeshakamilika.

Alisema kuwa katika mchezo huo, timu yake ilitengeneza nafasi tatu hadi nne za kufunga mabao kipindi cha kwanza lakini hazikuweza kutumiwa vema huku akisema kuwa mambo yatabadilika baadaye na timu hiyo kuweza kufunga nafasi wanazopata.

“Inahitajika kufanya kazi kubwa, kuna baadhi ya matatizo kwenye ushambuliaji kwa baadhi ya washambuliaji, nitafanya kazi kila siku na ninawaamini wachezaji wangu watafika kiwango cha juu na hapo baadaye kuweza kufunga mabao na kila mmoja kufurahia,”alisema.

Aidha alisema kuwa anaiamini timu yake na kama ikiendelea kucheza kwa namna hii na kila mmoja kufika mazoezini na kufanya kwa nguvu na kwa umakini na kushika kile anachowafundisha na kucheza kwa kiwango kikubwa zaidi ana uhakika watachukua pointi tatu kwenye mchezo huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad