HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, February 28, 2017

NAIBU WAZIRI ENG. NGONYANI ARIDHISHWA NA KASI YA UTENDAJI WA TBA

 Muonekano wa baadhi ya Nyumba zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam zikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), Arch. Elius Mwakalinga, akifafanua hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa nyumba kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, alipokagua maendeleo ya ujenzi wa nyumba hizo jijini Dar es Salaam.
 Muonekano wa moja ya mtungi wa kutengenezea gesi ukaa (Biogas), inayoendelea kujengwa katika Nyumba zinazojengwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), eneo  la bunju jijini Dar es Salaam. Gesi hiyo itatumika kutoa huduma kwa wakazi wa eneo hilo.
 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), Arch. Elius Mwakalinga (wa tatu kulia), akimuonyesha  Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani, hatua iliyofikiwa kwenye ujenzi wa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam zinazojengwa na Wakala huo.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani wa pili kulia), akitoa maelekezo kwa Uongozi wa Wakala wa Majengo Nchini (TBA), alipokagua maendeleo ya ujenzi wa hosteli za wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar  es Salaam. Kulia ni Meneja Kikosi cha Ujenzi cha TBA, Arch. Hamphrey Killo.
Muonekano wa moja ya jengo la hosteli ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambalo limekamilika na majengo hayo yataanza kutumika wiki ijayo kufuatia ujenzi wake kukamilika.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani ameupongeza Wakala wa Majengo Nchini (TBA),  kwa jitihada wanazozifanya katika kuongeza mapato na kununua vifaa vipya na kisasa vitakavyowezesha wakala huo kumudu ujenzi wa miradi mingi mikubwa kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi wa nyumba 851 ulioko Bunju nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam na mabweni ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Eng. Ngonyani ameeleza kuridhishwa kwake na mabadiliko makubwa ya utendaji yanayoendelea katika wakala huo.
“Nawapongeza kwa kazi nzuri ya ujenzi wa nyumba za kisasa za makazi ya watu, ongezeni ubunifu ili  nyumba zote zinunuliwe na kuwawezesha Watanzania kupata makazi bora kwa bei nafuu’ amesema Eng. Ngonyani.
Ameitaka TBA kuhakikisha inapata faida ili kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali kama ilivyo kwa taasisi nyingine za Umma na hivyo kuiwezesha Serikali kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
‘Ongezeni kasi katika ukusanyaji wa madeni kwa watu binafsi wanaokaa kwenye nyumba zenu na sisi Wizarani tutawasaidia katika kuhakikisha mnalipwa kwa wakati kwa wadaiwa wa Serikalini’ amesisitiza Eng. Ngonyani.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo ameelezea kuridhishwa kwake na kasi ya TBA katika ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo yanatarajiwa kukabidhiwa kwa chuo hicho wiki ijayo.
Mbweni hayo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 3,840 yamejengwa na TBA katika kipindi kisichozidi  miezi sita na yamegharimu takribani shilingi bilioni 10.
Naye Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Elius Mwakalinga amemhakikishia Naibu Waziri Eng. Ngonyani kuwa Wakala huo umejiimarisha kwa kuwa na vifaa vya kisasa na watendaji wenye sifa hivyo Serikali iendelee kuuamini na kuupa miradi mingi ya ujenzi wa nyumba na ofisi.
“Tunao wahandisi 74, wachoraji ramani 66, wakadiriaji majenzi 52 na bado tunao wataalam mbalimbali kutoka kwenye vyuo vikuu nchini wanaowezesha wakala wetu kuwa imara wakati wote’ amesema Arch. Mwakalinga.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yuko katika ziara ya siku mbili ya kukagua miradi mbalimbali ya ujenzi inayosimamiwa na Wakala wa Majengo Nchini (TBA) jijini Dar es Salaam.


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad