HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 30, 2017

SERIKALI YATENGA SHULE 55 , YAUNGA MKONO JITIHADA ZA TFF KUINUA MICHEZO

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kwamba inaunga mkono juhudi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika programu za maendeleo ya vijana, hususani nia yake ya dhati kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki itakayofanyika Tokyo, Japan mwaka 2020.

Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari aliyasema hayo mara baada ya kusikia program za TFF kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na Makamu Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Henry Tandau katika hafla ya uzinduzi wa kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki.

“Nimesikia program mbalimbali za TFF, naona zinakuja wakati mwafaka. Nimewapongeze kwa mipango yenu mizuri kwa sababu inaleta matumaini. Jambo kubwa ambalo linanisukuma na kuwapongeza ni kuwa na program ya vijana, hatuwezi kufanikiwa kama hatutakuwa na program ya vijana," amesema Omary. Serikali inatambua haya yote mnayofanya. Na ili kuboresha, Serikali imetenga shule 55 ambazo zitakuwa ni maalumu kwa ajili ya vijana, lengo ni kupata vipaji bora ambavyo vitakuwa vikiendelezwa, huku wakiwa wanapata elimu.

Aliendelea, kusema kuwa anasikia  TFF wameunda Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu hususani vijana ni jambo zuri, lakini rai yangu ni kwamba watakapounda kamati ya mfuko huo wawe watu wenye heshima ili wananchi waipende na ikiwa hivyo itafanikiwa wao kama Serikali watafanya kazi bega kwa bega na kamati hiyo na jambo kubwa ni kwamba lazima wakutane mara kwa mara.

Kabla ya Mkurugenzi Singo kuzungumza, Makamu Rais wa TOC, Ndugu Tandau, alipongeza pia harakati za kuanza mapema akisema: “Shukrani TFF kwa kuthamini TOC. Ni vizuri tumeanza mapema. Michuano ya Olimipiki ni mikubwa na inahitaji timu zenye viwango vya juu kufanikiwa kufuzu.”

Alieleza hadhara iliyohudhuria hafla hiyo, kuwa TOC inakuwa na Mawasiliano ya maandalizi Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki inayoitwa ‘Olympic Solidarity Program’ ambayo hutoa sehemu ya fungu ya maandalizi na kwamba TFF haina budi kuwasilisha program yake kwa ajili ya kuingia kwenye bajeti ambayo inaitwa ‘Team Support Grant’.

Awali kabla ya viongozi hao kuzungumza, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kinachofanywa sasa na Shirikisho si kutafuta miujiza kwenye matokeo badala yake ni kujenga timu (Maandalizi) kwa dhana kwamba Timu za Taifa haziokotwi kama embe dodo.“Mhe. Mkurugenzi, kujenga timu hizi ni gharama kubwa. Hata matunda ambayo tunasubiri moshi mweupe ya timu ya vijana, hayakutokea hivi hivi ni maandalizi. Si ajabu kabla ya mwisho wa wiki hii tukaona moshi mweupe,” alisema Malinzi.

Alisema ili vijana wa Tanzania waweze kufanya vema, hakuna budi wadau wakiwamo Serikali, Kampuni, Mashirika ya umma na watu binafasi kusapoti mbio hizo za kwenda Tokyo, Japan pamoja na timu nyingine za taifa. “Program nzima ni gharama kubwa,” Kadhalika, ili kutekeleza program hiyo, Rais Malinzi alizungumzia utulivu katika kufanya kazi kwa sasa kwa kuwa historia inaonesha kuwa kumekuwa na nia ovu ya baadhi ya wadau kutaka kutibua mambo mazuri yanayofanywa na uongozi wa mpira wa miguu.


 Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki 2020 na kuipongeza Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzaniana nchini  kwa  juhudi za kuandaa programu za maendeleo ya vijana.




 Rais wa    Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) Jamal Malinzi akizungumza wakati wa  uzinduzi wa kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki 2020 na kuwataka wadau wa michezo kuunga mkono jitihada zake na wasimuache peke yake katika kulisongesha gurudumu la michezo.
  Picha ya pamoja ya viongozi wa mpira wachezaji wa timu ya vijana  sambamba na Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Omari.
Wachezaji watimu ya vijana wakiwa katika mazoezi leo wakati wa  uzinduzi wa kampeni maalumu za kuifanikisha Tanzania kushiriki michuano ijayo ya Olimpiki 2020.Picha na Zainab Nyamka.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad