HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 30, 2017

MWANDISHI WA HABARI LEO AULA KAMATI YA UTENDAJI CHAMA CHA WAAMUZI

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

MWANDISHI wa Gazeti  la HabariLeo na SpotiLeo, Rahel Pallangyo amechaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya Utendaji  wa Chama cha Waamuzi wa Soka Mkoa wa Dar es Salaam kuwakilisha wanawake.

Rahel ambaye pia ni kocha mwenye leseni B inayotambuliwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) alimwangusha mpinzani wake Isabela Kapera ambaye ni mwamuzi mstaafu wa FIFA aliyepata kura moja dhidi ya tano za Rahel.

Nafasi ya Mwenyekiti ilikwenda kwa Omar Abdulqudir aliyepata kura tano na Makamu Mwenyekiti ni Sijali Mzeru aliyepata kura sita na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa alichaguliwa Jovin Ndimbo kwa kura sita.

Katibu Mkuu alichaguliwa Said Mbwana kwa kura tano, msaidizi ni Waziri Hunda aliyepata kura sita na Mhazini ni Job Wandiba aliyepata kura sita.

Awali akizungumza kwa niaba ya wenzake wa uongozi uliopita muda, Hemed Nteza alishukuru kwa ushirikiano wa wajumbe na wachama kipindi chote walichokaa madarakani na kuwaasa watakaochaguliwa kuendeleza umoja.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Victor Mwandike alishukuru kwa kufanikisha uchaguzi kufanyika na kushukuru wajumbe wa mkutano kamati yake kwa kushirikiana vema.

"Nashukuru wajumbe na mwanasheria wa kamati kwa kutusaidia kutafsiri vifungu vya katiba na hatimaye tumemaliza kazi, nawatakia kila la heri katika kutekeleza majukumu yenu," alisema Mwandike.

Katika hatua nyingine  Mwenyekiti mpya, Abdulqudir  aliwateua Hemed Nteza na Mzee Malipula kuwa wajumbe wa heshima wa kamati ya utendaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad