HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 16, 2017

MBARAWA AAGIZA TAASISI NCHINI KUJIUNGA NA KITUO CHA KUMBUKUMBU (IDC)

 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akisisitiza jambo wakati alipofanya mazungumzo na wafanyakazi ( Hawapo pichani) wa kituo cha Taifa cha kuhifadhia kumbukumbu Data Center kilichopo Kijitonyama jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati) akitoa maelekezo kwa Afisa Mkuu wa Ufundi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Senzige Kisenge (wa kwanza kulia), wakati alipokagua huduma za mkongo wa Taifa katika ofisi za Kampuni hiyo, Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Ufundi wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), Senzige Kisenge, namna Mkongo wa Taifa unavyofanya kazi nchini wakati alipokagua huduma za mkongo huo jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kushoto) akizungumza na mmoja wa watoa huduma wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) wakati alipokagua huduma za Kampuni hiyo, Jijini Dar es salaam.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Kulia) akizungumza na mteja (kushoto) aliyetembelea ofisi za huduma kwa wateja za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), ili kujipatia huduma zitolewazo ofisini hapo. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Waziri Kindamba.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa mmoja wa wateja waliotembelea kituo cha huduma kwa wateja cha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ili kujipatia huduma zitolewazo katika duka hilo.
 Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Wa pili kulia) akisikiliza maoni kutoka kwa wateja waliotembelea kituo cha huduma kwa wateja cha Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ili kujipatia huduma zitolewazo katika duka hilo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameziagiza Taasisi zote za Serikali nchini kuhakikisha zinaleta taarifa zao kuhifadhiwa katika kituo cha Taifa cha Kuhifadhi kumbukumbu cha Kijitonyama (IDC) kwani kituo hicho ni salama na kina ubora wa hali ya juu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.
Aidha, amezitahadharisha baadhi ya Taasisi zenye mpango wa kujenga na  kuanzisha vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu kuacha mara moja mpango huo,  kwani kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya kituo hicho na kupoteza fedha za Serikali.
Hayo yamezungumzwa jijini Dar es salaam na Waziri huyo mara baada yakutembelea kituoni hapo na kupokea taarifa ya uendeshaji wa kituo hicho kutoka kwa Mkuu wa Kituo.
“Sioni sababu kwa Taasisi nyingine kutaka kujenga vituo vyao vya kuhifadhi kumbukumbu, Serikali imeshawekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki, hivyo taasisi zote nchini zinalazimika kutumia kituo hiki”,  amesema Profesa Mbarawa.
Sambamba na hilo amezisisitiza kampuni zilizo chini ya Wizara yake kuwa mfano wa kuigwa na taasisi nyingine nchini kwa kuwa wa kwanza kuleta taarifa zao kuhifadhiwa katika kituo hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kituo hicho Abdul Mombokaleo, amefanunua kuwa hadi sasa wameshafanikiwa kuunganisha wateja 13 kujiunga na kituo hicho na wengine zaidi ya 40 wapo katika mchakato wa kujiunga.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa ametembelea ofisi za Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) na kusema kuwa ameridhishwa na utendaji wa kampuni hiyo kutokana na jitihada zake za kuteka soko la ushindani katika makampuni ya mawasiliano nchini.
“Nimefarijika zaidi kuona sasa TTCL inafanya vizuri katika eneo la masoko kwani nimeshuhudia matangazo mengi barabarani, kwenye luninga, magazetini na katika mitandao ya kijamii, hii inadhihirisha sasa mna mpango wa kuifufua kampuni hii”, amefafanua Profesa Mbarawa.
Ameutaka uongozi wa kampuni hiyo kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa uadilifu na ushirikiano ili kuleta mabadiliko chanya yatakayoboresha kampuni hiyo na kuteka zaidi soko la mawasiliano nchini.



Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad