HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, January 17, 2017

Afcon ilituhitaji Tanzania na itatusubiri Cameroon 2019- 1

Na Kelvin Lyamuya

WIKIENDI ya soka ilitukuta pale Libreville, Gabon kabla ya utamu wake kumalizikia Old Trafford, Manchester, England. Barani kwetu, Afrika, Pierre-Emerick Aubameyang akiwa kama nahodha mkuu wa timu ya taifa ya soka ya Gabon, aliwakaribisha mastaa wenzake katika Fainali za Mataifa Afrika.

Ni michuano ya kumsaka bingwa wa Afrika. Karibu Afrika!
Nilimkumbuka babu Hassan Shehata, mkongwe wa soka la Afrika aliyewapa Misri mataji matatu mfululizo ya michuano hiyo, 2006, 2008 na 2010.

Hivi sasa hayupo Misri tena, lakini ni kocha nitakayemkumbuka kwa jinsi alivyoudhihirisha umwamba wake pale Luanda, Angola kwa kuiangusha Ghana na kutwaa taji la tatu na la kihistoria, shukrani kwa bao pekee la kihistoria la Mohamed Nagy ‘Gedo’. 

Misri imeingia michuano ya mwaka huu ikiwa na nia ya kurudisha ubabe wao, je wataweza? Tusubiri.

Hiyo ni Afcon 2017, lakini wakati Watanzania hawajakaa sawa, wakashitushwa kama sio ‘kuduwazwa’ kwa taarifa ya msanii wetu mkubwa, Nasibu Abdul ‘Diamond Platinumz’ kukabidhiwa bendera ya taifa kwa ajili ya kwenda kutumbuiza pale Libreville.

Hoja na maoni kedekede yalitolewa na kila mtu alizungumza kile akijuacho. Andiko la leo halitagusia sana Afcon ya mwaka huu wala suala la bwana Diamond bali litaangazia makundi ya kufuzu Afcon 2019 itakayofanyika nchini Cameroon.

Droo yenyewe ilifanyika Gabon na timu kugawanywa kwenye makundi 12, nani kuumana na nani ni kuanzia Juni hadi kufikia Novemba 2018. Taifa Stars nayo ipo ikiwa imepangwa kundi L pamoja na mataifa ya Uganda, Lesotho na Cape Verde.

Baada ya wadau wa soka kuiona timu yao pendwa, wakaanza kutoa maoni wengi wao wakijipa matumaini makubwa na kundi hilo, sababu kuu; ‘timu zilizopo sio ngumu kiviile!’

Kwa lugha nyepesi tunaweza kusema sio timu ngumu lakini tusizidharau kiasi hicho kwani ni timu zilizopo juu yetu kwenye viwango vya FIFA (ukanda wa Afrika na duniani).

Na kuwa huko juu yetu pia kusiwe sababu ya kutuvunja nguvu kwani tunaweza kufanya vema na kusonga mbele, lakini tukumbuke kundi halitakuwa jepesi kama tuwazavyo ila litahitaji utayari wetu kwani michuano hiyo bado inazihitaji nchi kama Tanzania.

Hata hivyo, yapo ya msingi ambayo tumekuwa tukihimizana ili kuhakikisha Stars inashiriki Afcon na tutaendelea kushirikiana juu ya hilo kwani ni timu yetu sote na inatakiwa kuwemo huko.

Wale wasemao kwamba ni kundi jepesi wana hoja zao, lakini vijana wetu hawana budi kuifanya kazi ya kuliwakilisha taifa kwa umakini mkubwa zaidi ili kuhakikisha tunaipata nafasi hiyo ya kipekee tunayoisaka kila kukicha.

Tayari wadau mbalimbali wa soka wameshajiapiza kutoipa ushirikiano Taifa Stars iwapo itashindwa kufuzu Afcon 2019, japokuwa ni sie tu ambao tuliamini tungeweza kufuzu michuano ya mwaka huu na sio kwingineko waliotuzungumzia.

Lakini hata kama wakijiapiza hivyo, bado ni jukumu letu sote kuwa nyuma ya timu yetu ya taifa.

Ipo haja ya Shirikisho la soka nchini, TFF, kuchukua jukumu zito la kuisapoti timu kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hiki ni kipindi kigumu kwa vijana wetu, wanahitaji kufanyiwa mengi yatakayorudisha morali yao bila kusahau ushirikiano kutoka kwa Watanzania kwa ujumla.

Hakuna mafanikio yanayokuja bila maandalizi thabiti, ipo haja kwa kikosi chetu kufanya maandalizi ya kueleweka na maandalizi hayo yafuatane na kutambua nini kinachohitajika kwa sasa na baadae.

Je, tunataka kuishuhudia timu yetu ikibaki nchini kila mwaka? Je, tuko radhi kuilaumu Stars huku ikiwa nyumbani badala ya kuilaumu ikiwa Afcon pale Cameroon?

Wadau tuendelee kuipenda timu yetu, tuwape moyo wa kufika mbali.  TFF na wizara husika hakikisheni mikakati ya maendeleo ya Stars mnaifanyia kazi na kama haipo iwekeni kwa kushirikiana nasi wadau ili Afcon siku moja ijumuishe mataifa ya kutosha kutoka Afrika mashariki na sio Uganda pekee.

Wiki ijayo, nitazielezea changamoto tutakazozibeba katika kundi letu, na mengineyo…

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad