Katika siku za hivi karibuni kumeendelea kuwepo kwa vitendo na tabia
ya baadhi ya wananchi kujichukulia
sheria mkononi kwa kuwapiga, kuwachoma moto na kuwaua baadhi ya watu wasio na hatia pamoja na wanaoshukiwa
kujihusisha na vitendo vya kihalifu
jambo ambalo ni kinyume cha sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Mpaka sasa takwimu
za makosa ya kujichukulia sheria mkononi yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi
katika kipindi cha Januari hadi Agosti mwaka 2016 ni matukio 705 . Katika matukio hayo yaliyoripotiwa, Jeshi
la Polisi nchini limefanikiwa kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa
393.
Kufuatia hali hiyo, Jeshi la Polisi nchini linatoa
onyo kali kwa wote wenye tabia ya kujichukulia sheria mkononi kuacha
mara moja, Aidha, kwa kuzipuuza sheria za nchi zilizopo na wakati mwingine
kuzikiuka kwa makusudi na mbaya zaidi baadhi yao kufikia hatua ya kuwaua watu
wasio na hatia kwa hisia. Mwananchi yeyote anapaswa kutoa taarifa kwa vyombo vya
dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mhalifu au mtu yeyote
wanayemtilia mashaka katika maeneo yao.
Aidha, Jeshi la
Polisi nchini, litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa kufuatilia na
kuwakamata watu wote wanaojihusisha na tabia za kujichukulia sheria mkononi.
Jeshi la Polisi linatoa
wito kwa watu wote wakiwemo wenye ushawishi mkubwa katika jamii kuendelea
kukemea na kutoa elimu juu ya madhara ya kujichukulia sheria mkononi na badala
yake wananchi kuendelea kutii na kufuata sheria za nchi zilizopo.
Imetolewa na:
Advera Bulimba - ACP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
No comments:
Post a Comment