Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Kutoka kwa Mwenyekiti Mwenza na Mwenyekiti wa Masula ya Uhusiano wa Kimataifa wa Taasisi ya The Investment Climate Facility for Africa (ICF), Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, Ripoti ya Hali ya Hewa Barani Afrika, kwenye hoteli ya Serena jijini Dar Septemba 1, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Afrika wajiulize
wanaweza kuchangia kitu gani katika kuboresha maisha ya mamilioni ya
wakazi wa bara hilo.
Ametoa kauli hiyo jana usiku
(Alhamisi, Agosti 31, 2016) wakati akizungumza na wawakilishi wa taasisi
za kimataifa waliohudhuria uzinduzi wa taarifa ya Taasisi ya Kuboresha
Mazingira ya Uwekezaji barani Afrika (ICF) uliofanyika kwenye hoteli ya
Serena jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa
mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo alisema taasisi hiyo imesaidia kukuza
uwekezaji kupitia miradi katika nchi mbalimbali za Afrika kwa kuimarisha
mifumo ya ukusanyaji kodi, usajili wa biashara za wajasiriamali na
upatikanaji wa leseni za biashara.
“Kutokana na kazi
inayofanywa na taasisi hii, hali ya uwekezaji katika nchi nyingi
imeimarika na bara la Afrika limekuwa mbia kwa wawekezaji kutokana na
ushirikiano baina ya Serikali za nchi husika na sekta binafsi. Uchumi wa
nyingi za Afrika umeimarika kuliko hapo awali,” alisema.
Akitoa
mfano, Waziri Mkuu alisema zaidi ya wajasiriamali 500 kutoka Tanzania
walipatiwa mafunzo kwa ushirikiano baina ya ICF, Serikali na ESAURP ili
kuwajengea uwezo waweze kufanya biashara zao kwa tija zaidi. “Mafunzo
hayo yaliwalenga wajasiriamali wadogo na wa kati ambao wanajihusisha na
uvuvi, biashara za rejereja na jumla kutoka mikoa ya Mwanza na Dar es
Salaam”.
“Kupitia mafunzo hayo, wajasiriamali hao
waliweza kusajili biashara, kurasimisha biashara zao, kuongeza mitaji na
kujua namna ya kutunza taarifa za biashara zao,” alisema.
Mapema,
Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu
ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya wananchi kubadili
mitazamo yao juu ya sekta binafsi kwani nayo ni muhimu katika ujenzi wa
uchumi kwa nchi yoyote ile.
“Watu wengi wanahisi kwamba
wawekezaji ni wabaya. Hii si kweli. Tunapaswa kujenga mazingira ya
kuwakubali kwa sababu wanakuja na mitaji yao na wao wanawakilisha
michango kutoka kwa mamilioni ya wafanyakazi kutoka kwenye nchi zao.
Hatupaswi kuwaona kwamba ni maadui,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo kumshukuru Rais Mstaafu wa Serikali ya awamu ya nne, Mhe.
Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kukubali kuiruhusu taasisi hiyo ya ICF
iweke makao yake makuu hapa nchini wakati ilikuwa imeshakataliwa
kufanya hivyo katika nchi nyingi ambako ilipeleka maombi yake.
Aliwataka
viongozi mbalimbali watumie uzoefu uliowekezwa na taasisi hiyo kwenye
uboreshaji wa mifumo ya mahakama na ukusanyaji kodi, utoaji wa leseni,
urasmishaji wa biashara za wajasiriamali wadogo.
“Tunayo
maeneo mengi ambayo tumefanya vizuri iwe ni katika TEHAMA, miundombinu,
mahakama au mambo ya forodha. Uamuzi ni wenu juu ya jambo lipi muanze
nalo katika kuboresha huduma ili kuharakisha maendeleo ya bara hili,”
alisema.
No comments:
Post a Comment