HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, September 9, 2016

TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA.


TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA.
Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:- 

KUPATIKANA KWA MALI ZA WIZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na maafisa wa Polisi wa Mkoa wa Iringa na Songwe kuanzia tarehe 04.09.2016 hadi 08.09.2016 lilifanya Operesheni ya pamoja katika mikoa hiyo baada ya watu wasiojulikana mnamo tarehe 07.08.2016 majira ya saa 17:00 jioni kuiba mali iliyokuwa ikisafirishwa ambayo ni sabuni aina ya Ayu na Duru katoni 4,850 na rangi ya ukutani ndoo 10 aina ya Kale Drdwa za ujazo wa kilogram 25 na pakiti 08 za rangi ya ukutani aina ya Kale Drdwa zenye uzito wa Kilogram 15 kila moja. Jumla ya mali yote iliyoibiwa ilikuwa na thamani ya Tshs. Milioni 69,323,000/=.

Mali hizo zilizokuwa zikisafirishwa kutokea Dar es Salaam kuelekea Lubumbashi nchini Kongo na Mfanyabiashara aitwaye CHAPELE JACKLINE (48) raia wa nchini Kongo.

Katika Operesheni hiyo maafisa wa Polisi wa Mikoa ya Iringa, Mbeya na Songwe walifanikiwa kukamata katoni 3,380 pamoja na ndoo 09 za rangi zilizokuwa zimeibiwa huko Mkoani Iringa eneo la Mavugano Mafinga. Mali hizo zilipatikana katika mikoa hiyo kama ifuatavyo:-

Mkoani Rukwa mjini Sumbawanga zilipatikana katoni 240 za sabuni
Mkoani Songwe katika mji mdogo wa Tunduma zilipatikana katoni 3,100 za sabuni.

Mkoani Mbeya eneo la Iyunga Viwandani katika Godown zilipatikana katoni 40 za sabuni pamoja na ndoo 09 za rangi ya ukutani aina ya Kale Drdwa.

Aidha katika Operesheni hiyo watuhumiwa watatu walikamatwa kuhusika katika wizi huo ambao ni:-
1. BOSCO KAMSHA (52) Mfanyabiashara na Mkazi wa Sae Mbeya
2. KENEDY CHISUNGA (38) Dalali na Mkazi wa Mwanjelwa Mbeya
3. KENEDY SAMBO (43) Mjasiriamali na Mkazi wa Manga Veta Mbeya.

Upelelezi unaendelea ili kuwabaini watu wengine waliohusika katika wizi huo pamoja na kukamata mali nyingine ambayo bado haijapatikana.


Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na tukio 01 la ajali ya kifo kama ifuatavyo:-

AJALI YA KIFO.
Mnamo tarehe 08.09.2016 majira ya saa 07:00 asubuhi huko Mtaa wa Mama John, kata ya Ruanda, tarafa ya Iyunga, Jiji na mkoa wa Mbeya. Gari lenye namba za usajili T.712 DDF aina ya Toyota Coaster ikiendeshwa na dereva SIKU JORDAN (40) mkazi wa Veta ilimgonga mpanda baiskeli mwanaume asiyefahamika, mwenye umri wa miaka kati ya 23 hadi 25 na  kusababisha kifo chake.  

Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa gari. Dereva amekamatwa, mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Upelelezi unaendelea.

WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wafanyabiashara kuacha tamaa ya kutaka utajiri wa haraka haraka kwa njia zisizo halali kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kujikuta wananunua bidhaa feki au mali za wizi na kujisababishia matatizo. Pia Kamanda KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. Aidha anaendelea kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini hasa kwa kufuata na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoepukika. 

Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad