HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, August 30, 2016

WAZIRI MBARAWA AFUNGUA KOZI MPYA YA MAFUNZO YA WAKUFUNZI WA MARUBANI

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amekitaka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), kuhakikisha kinatoa marubani waliobobea katika masuala ya usafirishaji wa anga na wenye uadilifu katika taaluma hiyo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa kozi za Urubani Chuoni hapo, Waziri Prof. Mbarawa amesema kuwa Sekta ya anga ina changamoto ya upungufu wa marubani pamoja na uadilifu kwenye sekta hiyo, hivyo ameutaka uongozi wa chuo kutoa mafunzo ambayo yatabeba taaluma iliyo bora na yenye uadilifu.

“Tunataka kuijenga Air Tanzania mpya ambayo ilijengwa kwa misingi ya uadilifu, na serikali ipo tayari kukijengea uwezo chuo hiki ili kitowe marubani waadilifu watakaoweza kufufua shirikia letu la ndege”, amesema Waziri Mbarawa.
Rubani Focus Mmbaga kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), akitoa maelezo ya namna ndege inavyoendeshwa kwa kutumia kifaa maalum cha mafunzo ya urubani (simulator) kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam. 

Profesa Mbarawa amefafanua kuwa suala la uadilifu ni la muhimu, hivyo ameutaka uongozi wa Chuo na wakufunzi wake kuwa mfano kwa kuonyesha uadilifu ili wanafunzi watakaofuzu wawe na tija na uzalendo.

Aidha, amesema kuwa Serikali ina mpango wa kukiongezea uwezo chuo kwani lengo ni kuzalisha wataalamu wa usafiri wa anga ndani ya nchi na si kutegemea nchi nyingine. “Tunataka marubani waweze kupata mafunzo ndani ya Tanzania na ikitokea wameenda nje ya nchi basi iwe nikwaajili ya mafunzo maalumu tu” amesisitiza Profesa Mbarawa.

Waziri Profesa Mbarawa amesema kuwa kwa kutambua changamoto zilizopo kwenye sekta ya anga, Serikali imejipanga kuboresha sekta hiyo kwa kuongeza idadi ya ndege za abiria ambapo mbili zimekwisha nunuliwa na mbili nyingine zipo kwenye mchakato wakununuliwa ili kuongeza ufanisi wa shirika la ndege nchini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendesha ndege kwa kutumia kifaa maalum cha kufundishia marubani (simulator) kwenye chumba cha mafunzo kwenye Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).

Amewataka watanzania kuiamini Serikali yao kutokana na uamuzi wa ununuzi wa ndege mpya aina ya Bombadiat Q400 kwani Tanzania si ya kwanza kuzitumia bali kuna nchi nyingi zinazotumia ndege hizo ikiwemo Afrika ya kusini, Malawi, Rwanda, Ethiopia na Austria.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho Profesa Zacharia Mganilwa ameiomba serikali kuangalia jinsi ya kuongeza mikopo kwa wanafunzi wanaochukua kozi hiyo kutokana na umuhimu wake kwa jamii na Taifa kwa ujumla ili kuwezesha watanzania wengi kupata fursa ya mafunzo hayo.

Aidha, uongozi wa chuo hicho umeishukuru serikali kwa mpango wake wa uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafiri wa anga ili iweze kukuza na kuleta ushindani wa usafiri huo nchini.
Mkuu wa chuo cha Taifa cha Usafirishaji Profesa Zacharia Mganilwa akizungumza na wadau wa sekta ya usafiri wa anga (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo kwa wadau wa sekta ya usafiri wa anga (hawapo pichani) katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.
wadau wa sekta ya usafiri wa anga wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa katika uzinduzi wa mafunzo ya wakufunzi wa marubani uliofanyika jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad