Hussein Makame-MAELEZO
Watu 14 wamefariki dunia katika wilaya za Chemba mkoani
Dodoma na Kiteto mkoani Manyara kutokana na ugonjwa
unaojulikana kitaalamu kama ‘Aflatoxicosis’ unaosababishwa na
sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka iliyoharibika.
Hayo yamesema na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati akitoa taarifa kwa
waandishi wa habari juu ya magonjwa ya milipuko na magonjwa
mengine leo jijini Dar es Salaam.
“Ugonjwa uliosababishwa na sumu kuvu (Aflatoxins) uliripotiwa
kwa mara ya kwanza tarehe 13 Juni, 2016 katika wilaya za
Chemba mkoani Dodoma na baadaye mkoani Manyara katika
wilaya ya Kiteteo” alisema Waziri Ummy na kuongeza kuwa:
“Wagonjwa walikuwa na dalili za kuumwa tumbo, kuharisha,
kutapika, tumbo kuvimba na kuwa manjano sehemu mbalimbali
za mwili ambayo inaashiria kuathirika kwa ini”
Alisema mbali na vifo hivyo, hadi kufikia Julai 31 mwaka huu
wagonjwa 54 waliripotiwa kuugua ugonjwa hu huku wagonjwa
wanne wakilazwa kutokana na kuugua.
“Hadi kufikia tarehe 31, Juni 2016 kulikuwa na wagonjwa 54 na
watu 14 walipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.Aidha
katika wiki iliyopita aliripotiwa mgonjwa mmoja mpya kutoka
wilaya ya Kondoa” alisema Waziri Ummy na kufafanua kuwa:
“Jumla ya wagonjwa waliolazwa wodini ni wanne kati yao
mmoja yupo Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na watatu wapo
katika Hospitali ya Kondoa”
Waziri Ummy alitaja wilaya zilizoripoti wagonjwa hao na idadi
ya wagonjwa kuwa ni wilaya ya Chemba wagonjwa 38, Kondoa
wagonjwa tisa , Kiteto wagonjwa watatu, Chamwino wagonjwa
wawili na Dodoma Manispaa mgonjwa mmoja.
“Vijiji vilivyoathirika zaidi na ugonjwa huo ni kutoka wilaya ya
Chemba ambavyo ni Kinkima, Itolwa, Mwailanje na katika wilaya
ya Kondoa ni kijijini cha Ubembeni” alisema Waziri Ummy.
Hivyo, aliitoa hofu familia iliyopoteza watu wanne katika kijiji
cha Mwaikuzabe na kusema vifo hivyo havihusiani na uchawi au
kuwekewa sumu bali ni chakula cha siku ile kilithibitika kwamba
kilikuwa na sumukuvu.
Kufuatia athari hizo Serikali itafanya uchunguzi wa kina katika
wilaya kumi za Chemba, Kondoa, Chamwino na Kiteto na wilaya
nyingine za mikoa ya Sindida, Dodoma na Manyara zinazopakana
na wilaya hizo.
Alisema uchunguzi huo unalenga kubaini hali ya usalama wa
vyakula vinavyotumiwa na jamii ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa
huo na kuwaathiri wananchi wengi zaidi wanaoishi katika wilaya
hizo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taifa wa Afya wa Wizara hiyo
Dkt. Fausta Mosha alisema wizara imeandaa vipepereshi vyenye
maelekezo yanayotoa elimu juu ya kijikinga kwa kuandaa
chakula kuanzia hatua ya uvunaji shambani hadi wakati wa kula.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Otilia Gowelle
alisema njia bora ya kupambana na ugonjwa huo ni kuukinga
kwa kuhakikisha sumu kuvu haizalishwi kutoka kwenye nafaka.
Akifafanua kuhusu udhibiti, Waziri Ummy alisema wanashirikiana
na Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi kutoa elimu kwa wananchi
juu ya njia sahihi ya uhifadhi na uandaaji wa chakula
utakaosaidia kupunguza kiasi cha sumukuvu kwa nafaka ambazo
hazijaharibika sana.
“Njia hizi ni pamoja na kuhifadhi nafaka zilizokauka vizuri na
kuchambua nafaka zilizoharibika (zilizooza, kuvunjika,
zilizobadilika rangi), kukoboa mahindi kabla ya kusaga au kuacha
kutumia nafaka zitakazoonekana kuharibika rangi” alisema.
Waziri Ummy alisisitiza Serikali kuendelea kuimarisha mikakati
ya kitaifa ya kupunguza uchafuzi wa sumukuvu katika vyakula,
ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa kupima sumukuvu katika
damu na choo kidogo miongoni mwa taasisi za ndani ya nchi.
Inaelezwa kuwa ugojwa wa‘Aflatoxicosis’unaosababishwa na
sumu kuvu (Aflatoxins) kwenye nafaka uliwahi kutokea nchini
Kenya mwaka 2004 na kusababisha vifo vya zaida ya watu 100
huku wengine 200 waliathirika.
No comments:
Post a Comment