HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, July 27, 2016

TBS yatoa onyo kwa wanaotengeneza vilainishi feki



Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam.
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetoa onyo kali kwa watu wanaozalisha mafuta ya vilainishi vya mitambo na magari visivyo kidhi viwango vya kitaifa na kimataifa, kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Dkt. Egid Mubofu amewaambia waandishi wa habari jana jijini hapa kuwa shirika hilo halitakuwa na mjadala kwa wale watakaobainika na kuwaonya waache mara moja.

“Hivi karibuni shirika lilifanya msako mkali wa mafuta ya vilainishi vya mitambo na magari visivyo na viwango na kufanikiwa kuyabaini katika wilaya za Temeke na Ilala,” alisema Dkt. Mubofu.

Alisema katika msako huo walikikamata kiwanda bubu wilayani Temeke na kukifungia na kwamba sheria itachukua mkondo wake.

Katika msako huo lita 12,296 za vilainishi vya injini zilikamatwa, lita 811 za vilainishi vya mifumo ya breki na kilainishi aina ya ATF lita 1,241; jumla vikiwa na thamani ya Tshs milioni 46.

Pia aliwataka wazalishaji na waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kuwapatia bidhaa bora watanzania.

Dkt. Mubofu aliwataka wananchi kususia bidhaa isiyo na alama ya ubora ya TBS kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

“Bidhaa za vilainishi na bidhaa nyingine zote zinapoingizwa nchini lazima zikaguliwe kwa kufuata viwango vinavyotakiwa,” alisema.

Alisistiza kuwa mtu yoyote anayezalisha au anayetaka kuzalisha ni lazima afuate taratibu za nchi.

Alisema shirika litaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana kwa karibu na vyombo vingine nchini kama Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) miongoni mwa vingine katika kudhibiti bidhaa zisizo na viwango.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Shirika linategemea sana ushirikiano wa wananchi katika kupata taarifa na kuwataka wanaoishi mipakani kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona bidhaa zinapita bila kufuata taratibu ili kubaini bidhaa hafifu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad