Ripoti ya Lishe ya Dunia 2016 kuzinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu (Pichani)kesho (Jumatano) jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Jukwaa la lishe Tanzania (PANITA) Bw. Tumaini Mikindo ambae taasisi yake kwa kushirikiana na UNICE, UN Reach, Feed the Children mashirika mengine wanaoratibu uzinduzi huo, amesema katika uzinduzi huo utakaofanyika hapa jijini, Makamu wa Rais anatarajiwa kuambatana na mawaziri kadhaa ambao wizara zao zinazohusika kwa karibu na maswala ya lishe.
“Uzinduzi wa ripoti hiyo yenye kichwa cha habari “Kutoka ahadi mpaka utekelezaji, tumalize utapiamlo ifikapo 2030’’ (From promise to impact. Ending Malnutrition by 2030) uzinduzi huo hapo kesho ni mwendelezo wa zinduzi ziliyofanyika katika majiji tofati duniani ikiwa ni pamoja na Beijing, Johannesburg, Nairobi, New Delhi, New York, Stockholm na Washington D.C na sasa ni Dar es salaam,’’ alisema Bw Mikindo.
Amesema ripoti hiyo ni zana muhimu katika jitihada za kutokomeza utapiamlo nchini kwa kuwa itatoa hali halisi ya lishe Dunia nzima kwa unahusisha nchi Zaidi ya 129 ulimwenguni. Ripoti hiyo iliyohaririwa na jopo la wataalamu wa lishe duniani wakiongozwa na Bwana Lawrence Haddad ambae ni mtafiti aliebobea kwenye masuala ya lishe na kinara wa lishe Duniani, Tanzania kama sehemu ya ripoti hiyo itapata nafasi ya kujipima na kuchukua hatua stahiki.
Zaidi, akitaja malengo ya ripoti hiyo Bw Mikindo alisema ni pamoja na kupitia na kutathmini maazimio ya kupunguza utapiamlo yaliyowekwa na nchi katika mkutano wa kwanza wa Lishe na uchumi uliofanyika London mwaka 2013, pia kuisihi serikali kuongeza muamko wa kisiasa kwenye masuala ya lishe na kuongeza rasilimali za ndani kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya Lishe nchini.
“Malengo mengine ni kuhamasisha uwajibikaji wa pamoja katika ngazi zote za utawala ambazo zitasaidia nchi kumaliza tatizo la utapiamlo na kusisitiza kuzingatiwa kwa malengo ya Baraza la Afya Duniani katika vita dhidi ya utapiamlo,’’ alitaja Bw Mikindo huku akibainisha kuwa ripoti hiyo imekuwa ikitolewa kila mwaka kwa miaka mitatu sasa.
Jukwaa hilo la lishe (PANITA) ni muunganiko wenye lengo la kuwakutanisha Asasi zote za Kiraia zinazohusika na lishe, waadishi wa habari, wanasiasa na makundi mengine kwa lengo la kuhamasisha jamii juu ya masuala ya lishe ilikutokomeza tatizo la utapiamlo katika jamii.
No comments:
Post a Comment